

Lugha Nyingine
Jamhuri ya Afrika ya Kati yaadhimisha siku ya Uhuru kwa kutoa wito wa kuunga mkono amani
Bendi ya jeshi ikiwa kwenye gwaride la kuadhimisha miaka 65 ya uhuru wa Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Agosti 13, 2025. (Str/Xinhua)
YAOUNDE, Agosti 13 (Xinhua) -- Rais Faustin-Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amewataka wananchi kuunga mkono juhudi za amani kwa heshima ya watu waliofariki wakipigania uhuru wa nchi hiyo. Akihutubia nchi nzima kwa njia ya televisheni kwenye mkesha wa siku ya 65 ya Uhuru, inayoadhimishwa kila Agosti 13, Rais Touadera amesema, “miongo iliyopita imekuwa na mapinduzi ya kijeshi, uasi, migawanyiko, usaliti, na uingiliaji wa mambo ya ndani, ambayo yametunyima haki yetu ya kuwa na utu.”
Amesema changamoto hizo zimeiwezesha nchi yake kufahamu umuhimu wa amani kwa maisha ya jamii, na nafasi yake katika mchakato wa maendeleo ya jamii na uchumi ya nchi. Pia amesema ili nchi iweze kuwepo, ni lazima walinde amani iliyopatikana kwa kushinda taabu kubwa na ambayo inaendelea kuwa moja ya mali muhimu kwa watu wa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Rais huyo pia amesema miaka 65 baada ya uhuru, kwa sasa Jamhuri ya Afrika ya kati inajenga nchi ya jamhuri ya saba ambayo itakuwa ya matumizi ya kidijitali badala mali au rasimali, yenye ugatuzi kamili, na iliyounganishwa kidijitali, katika jitihada za "kujenga thamani endelevu, fursa, na kuwa na athari kimataifa".
Maadhimisho ya siku ya uhuru yalifanyika huku kukiwa na gwaride na maandamano ya raia kote nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Nchi hiyo ilipata uhuru rasmi kutoka kwa Ufaransa Agosti 13, 1960.
Askari wa vikosi vya ulinzi wakiwa kwenye gwaride la kuadhimisha miaka 65 ya uhuru wa Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Agosti 13, 2025. (Str/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma