Sudan Kusini yatoa dozi ya pili ya chanjo ya surua kwa watoto

(CRI Online) Agosti 15, 2025

Waziri wa afya wa Sudan Kusini Sarah Cleto Rial amesema nchi hiyo imejumuisha utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ya surua (MCV2) katika ratiba ya kawaida ya utoaji wa chanjo ikiwa ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha kinga ya watoto na kuzuia mlipuko wa surua.

Bi. Rial ameeleza kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa huko Juba kuwa huduma za kawaida za utoaji wa chanjo husika zitatolewa katika vituo visivyohamishwa, maeneo mengine nje ya vituo vya afya, na vituo vinavyohamishwa.

Habari zinasema mpango wa dozi mbili za surua ni sehemu ya pendekezo lililotolewa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2017. Sudan Kusini imekuwa nchi ya 45 ya kutoa huduma ya dozi ya pili ya chanjo ya surua ya MCV2 barani Afrika, na inapanga kutoa dozi hizo kwa watoto wachanga nchini humo wenye umri wa miezi tisa na miezi 18 ili kuimarisha uwezo wao wa kinga.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha