Vifurushi 161 vya msaada vimedondoshwa kwa ndege Gaza huku idadi ya wanaokufa kwa njaa ikiongezeka

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 18, 2025

JERUSALEM/AMMAN -- Jeshi la Israel limesema jumla ya vifurushi 161 vilivyokuwa na chakula vilidondoshwa kwa ndege Jumapili katika Ukanda wa Gaza wakati wa operesheni ya kutoa msaada iliyotekelezwa na nchi tisa, huku njaa ikiendelea kuenea katika eneo hilo baada ya vita vilivyoendelea karibu kwa miaka miwili. Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Denmark na Indonesia zilijiunga na operesheni hiyo.

Wakati huohuo Jeshi la Jordan limesema kwenye taarifa yake kuwa takriban tani 106 za chakula na vifaa vya msaada vilidondoshwa wakati wa operesheni hiyo. Jeshi la Israel limesema operesheni hiyo iliratibiwa “kwa mujibu wa maagizo kutoka kwa viongozi wa kisiasa,” na kukanusha tuhuma kuhusu kuleta njaa kwa makusudi.

Jeshi hilo lilianza kuratibu udondoshaji wa vifurushi vya chakula mwishoni mwa mwezi Julai, baada ya shinikizo kubwa la kimataifa kutokana na hali ya njaa iliyozidi kuwa mbaya kwenye eneo hilo.

Wataalamu na makundi ya msaada wametaja kuwa msaada huo ni mdogo, si salama na hauna ufanisi wa kuzuia kuenea kwa njaa, na kuitaka Israel kuruhusu malori zaidi ya utoaji msaada kuingia na kuwezesha kujengwa upya kwa mfumo wa afya wa Gaza, ambao umeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Israel.

Mamlaka za afya za Gaza zimesema njaa inaenea, na hospitali zimeripoti vifo saba katika saa 24 zilizopita, wakiwemo watoto wawili, kutokana na njaa na utapiamlo. Idadi hiyo imefanya jumla ya watu waliokufa kwa njaa hadi sasa kufikia 258, kati yao watoto wakiwa ni 110.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha