

Lugha Nyingine
Viongozi wa Ulaya na Zelensky kukutana na Trump mjini Washington
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen Jumapili amesema kwamba kutokana na ombi la Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, yeye na viongozi wengine wa Ulaya, pamoja na Rais Zelensky, watasafiri kwenda Washington leo Jumatatu kwa mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana siku ya Jumapili pamoja na rais Zelensky, von der Leyen alisema maamuzi kuhusu ardhi lazima yafanywe na Ukraine, na hayawezi kuchukuliwa bila Ukraine kuwepo mezani.
Alisisitiza kuwa Ulaya itaiunga mkono Ukraine hadi amani ya haki na ya kudumu ipatikane, na kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kuishinikiza Russia kidiplomasia na kiuchumi.
Pia alibainisha kuwa Umoja wa Ulaya unakaribisha kauli ya Marekani ya kuipa Ukraine uhakika wa usalama kama ilivyoelezwa kwenye Kifungu cha 5 cha Mkataba wa NATO, na kwamba Umoja huo uko tayari kuchukua majukumu yake yanayostahili ndani ya mfumo wa "Muungano wa Wenye Nia" kutoa usalama kwa Ukraine.
Ijumaa iliyopita, Rais Vladimir Putin wa Russia na rais Trump walimaliza mazungumzo yao katika mji wa Anchorage wa Marekani huko Alaska, lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa. Mazungumzo hayo yaliyochukua takriban saa tatu, yalilenga zaidi mzozo wa Ukraine, na pia kurekebisha uhusiano wa nchi hizo mbili ambao kwa kiasi kikubwa umekwama katika miaka ya hivi karibuni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma