China na UM zatoa wito wa kuboresha elimu ya ufundi stadi ili kuendeleza sekta ya viwanda barani Afrika

(CRI Online) Agosti 19, 2025

Maofisa wa China na Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuboresha elimu ya ufundi stadi na programu za kuendeleza watu wenye ujuzi barani Afrika, ili kuharakisha mchakato wa ukuaji wa viwanda na mageuzi ya bara hilo.

Wito huo waliutoa Jumapili kwenye ufunguzi wa semina ya usimamizi wa elimu ya ufundi stadi na ujenzi wa uwezo kwenye Karakana ya Luban huko Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kiongozi wa ujumbe wa China kwenye Umoja wa Afrika Jiang Feng amesema China imedhamiria kujenga jumuiya ya maendeleo ya elimu ya ufundi stadi barani Afrika kupitia programu mbalimbali za mafunzo ya ufundi. Semina hiyo ni hatua moja ya kiutendaji katika kutekeleza ahadi za chini ya mfumo wa Kituo cha Mfano cha Ushirikiano wa Pande Tatu za China, Afrika na Umoja wa Mataifa.

Ofisa programu wa Ethiopia katika Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) Asegid Adane Mebratu amesisitiza haja ya kuhimiza elimu ya ufundi stadi barani Afrika, ili kukidhi mahitaji yanayochipuka ya viwanda na jamii barani humo. Karakana ya Luban inaonyesha jitihada za kiutendaji ili kuimarisha maendeleo ya ustadi wa kiufundi na kuhimiza mawasiliano ya teknolojia yanayounga mkono kuinuka kwa viwanda na kuwaandaa wataalamu barani Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha