Katibu Mkuu wa UM apongeza wafanyakazi watoa misaada, na kutoa wito wa kuwalinda wakati wa Siku ya Ubinadamu ya Dunia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 20, 2025

Wapalestina waliopoteza makazi kutokana na mashambulizi ya Israel wanakabiliwa na changamoto ya kuishi katika hali ngumu kwenye mahema katika ufukwe wa Gaza, Agosti 18, 2025.

Wapalestina waliopoteza makazi kutokana na mashambulizi ya Israel wanakabiliwa na changamoto ya kuishi katika hali ngumu kwenye mahema katika ufukwe wa Gaza, Agosti 18, 2025.

UMOJA WA MATAIFA -- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres amesema wafanyakazi wa kutoa misaada, ambao wenyewe wanazidi kuteseka kutokana na mashambulizi, ndio watu wa mwisho wanaotegemewa kuokoa maisha ya zaidi ya watu milioni 300 wanaokumbwa na migogoro au maafa kote duniani.

Kwenye hotuba aliyotoa kwa njia ya video wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ubinadamu ya Dunia, Bw. Gutteres amesema, “mwaka jana, wafanyakazi watoa misaada wasiopungua 390 - ambao ni rekodi ya juu - waliuawa katika sehemu mbalimbali, kutoka Gaza hadi Sudan hadi Myanmar na kwingineko,” ameongeza kuwa “Sheria ya kimataifa iko wazi: watoa misaada ya kibinadamu lazima waheshimiwe na kulindwa. Na kamwe hawastahili kulengwa.”

Bw. Guterres amesema licha ya kuwa sheria hiyo haiwezi kujadiliwa na inabana pande zote kwenye migogoro, siku zote na kila mahali, sheria hiyo inakiukwa na hatua hazichukuliwi.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema Agosti 19 imekuwa inaadhimishwa kuwa Siku ya Ubinadamu Duniani tangu 2009 kwa sababu Agosti 19, 2003 wafanyakazi 22 wa Umoja wa Mataifa waliuawa na magaidi walioshambulia makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika Hoteli ya Canal mjini Baghdad.

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema wafanyakazi wengi watoa misaada waliouawa ni wafanyakazi wanaohudumia jamii zao, kushambuliwa wakiwa kazini au majumbani mwao. Huko Gaza, mwaka 2024 wafanyakazi 181 watoa misaada ya kibinadamu waliuawa, ambayo ni idadi kubwa zaidi duniani, wakati nchini Sudan, wengine zaidi ya 60 walipoteza maisha.

OCHA imesema kuwa huko Gaza, wafanyakazi 520 wa kutoa misaada, wengi wao wakiwa ni wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, linalojulikana kama UNRWA, wameuawa tangu kuanza kwa mgogoro wa Palestina Oktoba 2023, na kupafanya Gaza kuwa mahali pa hatari zaidi kwa wahudumu wa kibinadamu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha