Kenya yazitaka nchi za Afrika kuimarisha usalama mipakani na kuzuia ugaidi

(CRI Online) Agosti 20, 2025

Maafisa wa Kenya wamezitaka nchi za Afrika kuimarisha usalama wa mipakani kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu kama vile ndege zisizo na rubani na uchunguzi wa AI ili kuzuia mashambulizi ya kigaidi.

Wakizungumza katika Mkutano wa Nne wa Nairobi, ambao ni wa kikanda wa kukabiliana na ugaidi uliofanyika kwa siku mbili mjini Nairobi, Kenya, maafisa hao walisisitiza kuwa mipaka salama ni muhimu katika kuzuia wanamgambo wenye itikadi kali kufanya uharibifu kwa watu wa Afrika walio hatarini.

Mkutano huo wenye kauli mbiu "Kuimarisha Usalama Mipakani ili Kuzuia na Kukatiza Harakati za Kigaidi", uliwaleta pamoja maafisa waandamizi wa serikali, wataalam wa usalama, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wanachama wa asasi za kiraia na wasomi kutoka nchi 15 za Afrika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Kenya, Raymond Omollo, alisema ugaidi unaendelea kuwa tishio la kuvuka mpaka kote barani Afrika, na hivyo kuna ulazima wa kuimarishwa kwa uratibu, ufuatiliaji, na kupeana taarifa za kijasusi ili kuupunguza.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Kenya (NC), zaidi ya asilimia 80 ya vifo vinavyohusiana na makundi yenye itikadi kali barani Afrika vilitokea katika maeneo ya mpakani mwaka 2024, ambapo Afrika Magharibi ina ongezeko la mara kumi la mashambulizi ya kuvuka mpaka tangu 2020, huku biashara ya magendo katika Bahari ya Hindi ikiongezeka kwa asilimia 25 katika mwaka huo huo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha