Kwenye nyanda za Maasai Mara nchini Kenya, Wachina wawili wajengea mabinti 29 maskani yenye matumaini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 22, 2025
Kwenye nyanda za Maasai Mara nchini Kenya, Wachina wawili wajengea mabinti 29 maskani yenye matumaini
Wasichana wakicheza mpira kwenye Kituo cha Uokoaji cha Namunyak, katika mji wa Aitong wa Kaunti ya Narok, kusini-magharibi mwa Kenya, Agosti 31, 2025. (Xinhua/Yang Guang)

NAIROBI - Karibu kila wikendi, Tang Lin na Yuan Lin huvuka nyanda za Maasai Mara nchini Kenya, gari lao likiwa limepakiwa vifaa -- raba, nguo, peremende, na vitu muhimu vya kila siku – vikielekea kwa mabinti 29 walio chini ya uangalizi wao.

Pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara katika Kaunti ya Narok kuna kituo cha uokoaji cha Namunyak, kimbilio la wastani lakini muhimu kwa wasichana ambao awali mustakabali wao haukuwa na uhakika. Jina lake, Namunyak, linamaanisha "furaha" katika lugha ya Kimasai.

Tang na Yuan, wote kutoka Mji wa Chongqing, kusini-magharibi mwa China, walikwenda Kenya kwa mara ya kwanza kufanya mambo ya utalii. Kadri watalii Wachina wanaotembelea nchi hiyo ya Afrika Mashariki walivyozidi kuongezeka, biashara yao ilikua kwa kasi. Mwaka 2019, walipiga hatua kubwa na kununua nyumba ya kulala wageni katika Mbuga ya Maasai Mara. Kile kilichoanza kama mradi wa ujasiriamali punde kilichanua kuwa dhamira isiyotarajiwa ya huruma.

Muda mfupi tu baada ya kufungua nyumba yao hiyo ya kulala wageni, mwanamke mwenyeji aitwaye Mary Silantoi alikwenda kwao. Akiwa mtu wa kujitolea katika idara ya masuala ya wanawake na watoto ya kaunti hiyo, Silantoi alikuwa amechukua mabinti kadhaa ambao walitoroka ndoa za mapema au ukeketaji. Aliomba nafasi ya kuendesha duka dogo kwenye nyumba hiyo ya wageni ili kuunga mkono huduma na matunzo yao.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na serikali ya mtaa, mabinti wenye umri wa miaka 10 hadi 19 huchukua asilimia karibu 30 ya wanawake wajawazito katika eneo hilo. Wengi, wakiwa bado watoto wenyewe, wameozeshwa na familia zao kwa kubadilishana na ng'ombe wachache.

"Nina binti yangu mwenyewe. Nilipoona watoto wakikimbia bila kuvaa viatu na kujua kwamba wengi walikuwa nje ya shule, sikuweza kuangalia pembeni." anasema Tang mwenye umri wa miaka 48.

"Wenyeji walitusaidia kuanzisha biashara yetu, na tulitaka kurudisha kitu kwao," Yuan anasema.

Wawili hao waliamua si tu kuunga mkono duka la Silantoi bali pia kusaidia kujenga makazi ya kudumu, salama kwa mabinti hao. Uamuzi huo ulisababisha kuanzishwa kwa Namunyak -- shirika la kijamii lenye dhamira ya kulinda mabinti walio katika mazingira magumu.

Juni 2023, Tang na Yuan walinunua ekari 15 (hekta karibu 6) za ardhi karibu na Mji wa Aitong wa Narok na kujenga kile ambacho sasa ni kituo cha uokoaji cha Namunyak. Ingawa si kubwa, kituo hicho kilimpa Silantoi na mabinti hao mahali ambapo wanaweza kupaita pa kwao wenyewe.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Tang na Yuan wamekarabati makazi hayo ya mabinti, kuweka umeme na miundombinu ya maji, kulipia karo zao za shule, na kuajiri walinzi na wahudumu.

Karibu na kituo hicho kuna majengo mapya ya madarasa, jiko, na vyoo, pamoja na vibanda vitatu vya kijadi vilivyoezekwa kwa nyasi vinavyotumika kama ofisi ya Silantoi na nyumba za kuishi.

Mwezi Machi 2024, serikali ya mtaa iliisajili rasmi Namunyak kuwa shirika la kijamii, kwa kutambua mchango wake kwa ustawi wa wenyeji.

Kwa Tang na Yuan, safari yao nchini Kenya ni zaidi ya kutoa ufadhili. "Tumejenga biashara hapa, lakini pia tumejenga familia," Tang amesema. Yuan ameongeza, "Furaha inamaanisha kila binti -- iwe Kenya au China -- anaweza kuishi maisha mazuri."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha