Lugha Nyingine
Ufaransa yatambua Nchi ya Palestina kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya suluhisho la nchi mbili
UMOJA WA MATAIFA - Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema jana Jumatatu kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu suluhisho la nchi mbili kwamba nchi yake inaitambua rasmi Nchi ya Palestina, ikiungana na nchi nyingine nyingi za Umoja wa Mataifa ambazo tayari zimefanya hivyo.
"Ninatangaza leo kwamba Ufaransa inaitambua Nchi ya Palestina," Macron amesema kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi ya Juu kuhusu Utatuzi wa Amani wa Suala la Palestina na Utekelezaji wa Suluhu ya Nchi Mbili, ulioendeshwa kwa pamoja na Ufaransa na Saudi Arabia.
"Wakati umefika. Hatuwezi kusubiri tena," amesema, akiongeza kuwa "tunataka nchi mbili kuishi kwa amani na usalama."
Baada ya utambuzi huo wa Ufaransa, nchi zaidi ya 150 zimeshatangaza kutambua Nchi ya Palestina.
Siku ya Jumapili, Uingereza, Canada, Australia na Ureno ziliitambua rasmi Nchi ya Palestina ili kusukuma "suluhisho la nchi mbili," wakati Israeli ikiendelea na mashambulizi yake na kunyakua Gaza licha ya kulaaniwa kimataifa.
"Mgogoro kati ya Israel na Palestina haujatatuliwa kwa vizazi vingi," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kwenye mkutano huo uliofanyika siku ya ufunguzi wa Wiki ya ngazi ya juu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
"Mazungumzo yameshindwa. Maazimio yamepuuzwa. Sheria ya kimataifa imekiukwa," amesema.
Hali hiyo haiwezi kuvumilika, na inazidi kuzorota kila wakati, amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
Annalena Baerbock, Rais wa Mkutano Mkuu wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, amesema Baraza Kuu limekuwa wazi kabisa: "Tunahitaji usimamishaji vita wa mara moja, usio na masharti na wa kudumu mjini Gaza. Israel lazima mara moja iwezeshe uingiaji na uwasilishaji kikamilifu, kwa haraka, kwa usalama na bila vizuizi wa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Palestina. Hamas lazima iachilie huru mara moja na bila masharti mateka."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




