Mutharika ashinda urais Malawi, Rais Chakwera anayemaliza muda wake akubali kushindwa (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 25, 2025
Mutharika ashinda urais Malawi, Rais Chakwera anayemaliza muda wake akubali kushindwa
Watu wakisubiria matokeo ya uchaguzi wa rais kwenye Kituo cha Taifa cha Kuhesabia Matokeo mjini Lilongwe, Malawi, Septemba 24, 2025. (Xinhua/Peng Lijun)

LILONGWE – Rais wa zamani wa Malawi, Peter Mutharika ameshinda uchaguzi wa urais nchini humo kwa kupata asilimia 56.8 ya kura zote halali zilizopigwa, akichukua ushindi wa moja kwa moja dhidi ya rais anayemaliza muda wake Lazarus Chakwera, tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imetangaza jana Jumatano.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) Annabel Mtalimanja ametangaza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Lilongwe kuwa, Rais huyo mteule, aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (DPP), amepata kura takriban milioni 3.04 katika uchaguzi mkuu wa Septemba 16 uliokuwa na wagombea 17, wakati Chakwera wa Malawi Congress Party (MCP) amepata kura takriban milioni 1.77.

Awali siku hiyo ya Jumatano kabla ya kutangazwa matokeo hayo, Rais Lazarus Chakwera wa Malawi alitangaza kukubali kushindwa katika uchaguzi huo.

Akizungumza katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni jana Jumatano chini ya saa mbili kabla ya Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) kutangaza matokeo yake hayo ya mwisho ya uchaguzi huo, Chakwera pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru Wamalawi wote kwa uungaji mkono wao kwa miaka mitano iliyopita.

"Ni wazi kwamba mpinzani wangu mkuu, Mheshimiwa Profesa Arthur Peter Mutharika wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, alikuwa tayari amepata uongozi usioweza kushindwa na ndiye mshindi tarajiwa wa uchaguzi wa urais," Chakwera wa Chama cha Malawi Congress alisema.

“Kwa sababu hiyo, muda mfupi uliopita nilimpigia simu Profesa Mutharika moja kwa moja kumpongeza kwa ushindi wake wa kihistoria na kumtakia heri katika kipindi chake cha uongozi kuwa Rais wa saba wa Jamhuri ya Malawi,” amesema.

Pia ametumia fursa hiyo kuwashukuru waungaji mkono wake, akisema “nitawashukuru daima kwa kuniamini na kwa kuniunga mkono katika ugombea wangu," na kuwahimiza Wamalawi wote kuunga mkono juhudi za Mutharika kwa ustawi wa taifa.

Chakwera pia ameipongeza MEC kwa kile alichoeleza kuwa ni kazi ya kupongezwa katika kusimamia uchaguzi huo mkuu.

Mutharika, ambaye alikuwa rais wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, atarejea ofisini huku aliyekuwa Mwenyekiti wa MEC Jane Ansah akiwa makamu wake wa rais.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha