Lugha Nyingine
Mwanajeshi mstaafu wa Shenzhen, China aungana na wastaafu wenzake kufanya hisani, kuinua vipato vya wakulima wenyeji
Mwanajeshi mstaafu Huang Guocheng mwenye asili ya Kijiji cha Xiasha, Mtaa wa Shatou katika Wilaya ya Futian mjini Shenzhen, China amejipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa jamii na kupongezwa na serikali ya mtaa anaoishi kutokana na juhudi zake za kutoa hisani kwa wenye uhitaji na kuwezesha kuinua vipato vya wakulima wenyeji kupitia mkahawa wake aliouanzisha punde baada ya kustaafu.
Akiwa ni mtu wa kujitolea Huang yeye binafsi ameweza kushiriki katika shughuli za kujitolea zaidi ya mara 200, na pia ameweza kuongoza karibu watu 3000 kuingia kwenye kazi hiyo ya kujitolea.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Timu ya Kufanya Utafiti Kuhusu Shenzhen ya People’s Daily Online hivi karibuni kwenye mkahawa wake wa Shatou Four Seasons, Huang amesema kuwa yeye na wanajeshi wenzake wastaafu wamejiunga na kundi la kujitolea la serikali ya mtaa mjini Shenzhen kujitolea katika mambo mbalimbali ya kijamii, kutoa hisani kwa wenye uhitaji lakini pia kujitoa kwa hali na mali katika kusaidia wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni.
Huang ametoa mfano wa jinsi yeye na wanajeshi wenzake wastaafu wanavyosaidia wanafunzi wanaokuwa wakifanya mtihani wa Gaokao wa kuingia Chuo, ambao ni moja ya mitihani migumu unayofanywa kila mwaka na maelfu ya wanafunzi kote China ili kupata fursa ya kuingia elimu ya chuo.
Amesema, kila mwaka yeye na wenzake, hutoa magari yao kusafirisha wanafunzi kwenda kwenye vituo vya mitihani, kuhamasisha na kukodi madereva teksi mjini Shenzhen kushiriki zoezi hilo na pia kutoa huduma za chakula na mahitaji muhimu kwa wanafunzi kutoka familia duni wanaokuwa wakifanya mtihani huo.
Aidha, Huang kupitia mkahawa wake, amekuwa akiwatafutia kazi wanajeshi wenzake wastaafu, kununua mazao ya kilimo kutoka kwa wakulima wenyeji na hivyo kuongeza kipato chao maradufu, kushiriki shughuli za uchumi wa mzunguko kwa kuchakata taka na kwa ujumla kutumia mkahawa wake kama jukwaa la kuunga mkono wakulima na watu wahitaji.
"Mfano mmoja ni kwamba, mwaka huu, katika mahali paitwapo Maoming kulitokea mafuriko. Kwa hiyo wakulima wenyeji hawakuweza kuuza matunda yao ya shokishoki. Katika hali hii nilinunua matunda yao kuwasaidia kuyauza kwa uzani au kuyauza mezani kama mlo au zawadi ndogo kwa wateja wangu hapa. Niliwauzia jumla ya kilo 5000" amesema Huang.
Huang alianzisha Mkahawa wa Four Seasons kutoka kwenye biashara ya usiku ya kibanda cha vyakula. Juhudi zake zimeufanya mkahawa wake kuwa mkubwa na maarufu miongoni mwa wakazi wa mji wa Shenzhen hasa kutokana vyakula vyake vya ladha na aina mbalimbali hasa vya baharini.
Harakati zake za hisani na kujitolea kwa jamii, zimempa Huang tuzo mbalimbali. Mathalan, katika robo ya tatu ya mwaka 2024 alikuwa miongoni mwa watu wawili wa Shenzhen waliofika kwenye fainali ya shindano la “Watu Wakarimu wa China”.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




