Lugha Nyingine
China na Misri zachunguza vichocheo vipya vya ukuaji kwa ushirikiano wa uwekezaji
CAIRO - Maafisa waandamizi wa China na Misri, viongozi wa biashara na wawekezaji walikusanyika Jumapili kwenye Jukwaa la kwanza la Uwekezaji kati ya China na Misri lililofanyika Cairo ili kuchunguza vichocheo vipya vya ukuaji kwa ushirikiano wa uwekezaji.
Kwenye jukwaa hilo, Hassan El-Khatib, waziri wa uwekezaji na biashara ya nje wa Misri, amesisitiza dhamira ya nchi hiyo kupanua ushirikiano wa pande mbili kwenye uwekezaji na biashara katika maeneo mapana zaidi.
"Misri inatafuta uhusiano wa biashara na uwekezaji wenye uwiano kupitia kuvutia uwekezaji zaidi wa China na kupanua msingi wa uzalishaji wa pamoja kwa ajili ya mauzo ya nje," amesema El-Khatib.
Kwa upande wake, Ling Ji, naibu waziri wa biashara na naibu mwakilishi wa biashara ya kimataifa wa China, amesema kuwa China imeendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Misri kwa miaka 13 mfululizo, huku Eneo la Ushirikiano wa Kiuchumi na Biashara kati ya China na Misri la TEDA Suez likiwa limevutia kampuni karibu 200.
"Inatarajiwa kwamba China na Misri zitabaki kuwa marafiki muhimu na washirika wa kuaminika katika njia ya maendeleo, zikishirikiana kuhimiza ukuaji tulivu na mzuri wa ushirikiano wa uwekezaji kwa manufaa ya watu wa pande zote mbili," amesema.
Akisema kuwa China kwa sasa ni miongoni mwa wawekezaji wenye shughuli nyingi na ukuaji wa haraka zaidi nchini Misri, Balozi wa China nchini Misri Liao Liqiang amesema kuwa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja lililopendekezwa na China linaendana kwa karibu na Dira ya Misri ya 2030, ambayo imeleta matokeo yenye matunda katika ushirikiano wa kivitendo kati ya pande hizo mbili.
"Leo, wajasiriamali zaidi ya 100 wa China wako hapa, wakileta teknolojia mpya ya kisasa, uwezo wa hali ya juu wa viwanda, na shauku kubwa ya ushirikiano. Pia tunakaribisha kampuni za Misri kwenda China na kutafuta fursa" amesema Liao.
Likiwa limeandaliwa na Ubalozi wa China mjini Cairo, Mamlaka Kuu ya Uwekezaji na Maeneo ya Biashara Huria ya Misri, na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Misri, tukio hilo lililenga kujenga jukwaa la mawasiliano na uratibu, na kuchunguza kwa pamoja vichocheo vipya vya ukuaji kwa ushirikiano wa uwekezaji.
Likileta pamoja kampuni zaidi ya 200 za China na Misri, lilishirikisha mfululizo wa maonyesho na majadiliano ya jopo, yakiwemo mijadala ndogo kuhusu ushirikiano katika nyanja za nguo, nishati mpya na uchumi wa kidijitali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




