Lugha Nyingine
Maonyesho ya Teknolojia ya Afrika yaanza nchini Afrika Kusini kulenga mustakabali jumuishi wa kidijitali (2)
![]() |
| Watu wakitembelea Maonyesho ya Teknolojia ya Afrika 2025 mjini Cape Town, Afrika Kusini, Novemba 11, 2025. (Picha/cfp) |
CAPE TOWN – Maonyesho ya Teknolojia ya Afrika, Africa Tech Festival 2025 yameanza rasmi jana Jumanne mjini Cape Town, mji mkuu wa kibunge wa Afrika Kusini, yakikusanya wavumbuzi, watunga sera, na wawekezaji ili kuchunguza namna teknolojia inavyoweza kuendeleza mustakabali jumuishi wa kidijitali kwa Afrika.
Akihutubia hafla ya ufunguzi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Kidijitali wa Afrika Kusini Solly Malatsi amesema kuwa Afrika lazima ijenge misingi imara ya kidijitali ili kuhakikisha teknolojia zinazoibuka zinamnufaisha kila mmoja.
"Kama tunataka Afrika ifaidike na kushiriki katika wimbi lijalo la uvumbuzi, hasa AI, lazima tuweke misingi mitatu kwa kiwango kikubwa: muunganisho na vifaa vya bei nafuu; miundombinu ya kidijitali ya umma yenye uhakika; ujuzi wa matumizi ya kidijitali unaowafikia watu pale walipo," amesema Malatsi.
"Teknolojia zinazoibuka kama vile AI zitakuwa zana za fursa, na siyo alama za kutengwa. Tutageuza mifano kuwa bidhaa, na bidhaa kuwa thamani ya umma ili kujenga mustakabali wa kidijitali ulio jumuishi zaidi kwa bara letu," ameongeza.
Sasa yakifanyika kwa mara 28, Maonyesho hayo ya Teknolojia ya Afrika ni tukio kubwa zaidi la teknolojia na uvumbuzi wa kidijitali barani Afrika, ambayo yamepangwa kuendelea hadi kesho Alhamisi. Yanatarajiwa kuvutia wajumbe 17,000, waonyeshaji bidhaa 300, na wazungumzaji 450.
Maonyesho hayo yakifanyika chini ya kaulimbiu ya "Uvumbuzi Unaowajibika, Uwekezaji Jumuishi, Muunganisho kwa Maendeleo, na Sera zinazosawazishwa," yanajumuisha vipindi vinne ambavyo ni AfricaCom, AfricaTech, AfricaIgnite, na Mkutano wa AI Cape Town.
Meneja wa Kipindi cha AfricaCom Sean Suzuki amesema changamoto za miundombinu ya kidijitali barani humo bado zinaunganishwa na "upatikanaji na gharama ya muunganisho."
"Hii inahusiana na changamoto za kisheria, na ni muhimu pia kuendeleza mifumokazi sahihi vilevile; kujenga ushirikiano muhimu katika sekta ya TEHAMA; na pengo la ujuzi wa kidijitali," amesema.
Justin Georges Tala, meneja wa akaunti za kimataifa katika Shirika la Mawasiliano ya Simu la Cameroon, ambalo linahudhuria AfricaCom mwaka huu, amesema kupunguza pengo la kidijitali barani Afrika kunahitaji hatua za pamoja.
"Hatuwezi kufanya hili peke yetu -- lazima kuwe na ushirikiano wa kimkakati ambao utafanywa kuhakikisha tunapunguza pengo la kidijitali barani Afrika," amesema, akiongeza kuwa ushirikiano wa kimkakati unahitajika ili kutoa "muunganisho wenye maana wa mwanzo hadi mwisho" kwa bara nzima.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




