Jaji Okowa wa Kenya achaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 13, 2025
Jaji Okowa wa Kenya achaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock (kushoto) akiongoza mkutano wa Baraza Kuu kwa ajili ya kumchagua jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Novemba 12, 2025. (Evan Schneider/Picha ya UN/kupitia Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA – Jaji Phoebe Okowa wa Kenya amechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) jana Jumatano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Abdulqawi Yusuf wa Somalia, ambaye alijiuzulu kuanzia Septemba 30.

Okowa atashika nafasi hiyo katika kipindi kilichosalia cha Yusuf, ambacho kitaendelea hadi Februari 5, 2027. Ni mwanasheria wa Kenya na profesa wa sheria za kimataifa za umma katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London na amekuwa ni mjumbe wa Kamisheni ya Sheria ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Mkataba ulioanzisha ICJ, majaji huchaguliwa kwa kura ya siri katika Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ili kuchaguliwa kuwa jaji, mgombea lazima apate wingi wa kura kamili katika mabaraza yote hayo mawili, ambayo hupiga kura kwa wakati mmoja lakini katika mazingira tofauti.

Kulikuwa na wagombea wanne waliowania nafasi hiyo. Okowa ameshinda baada ya raundi tatu za kupiga kura kwenye Baraza la Usalama na raundi nne za kupiga kura kwenye Baraza Kuu.

ICJ yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi ina majaji 15 wanaochaguliwa kwa kipindi cha miaka tisa. Majaji wanaweza kuchaguliwa tena baada ya kipindi chao kuisha.

Kama ikitokea jaji kufariki au kujiuzulu wakati wa kipindi chake madarakani, uchaguzi maalum utafanyika ili kumchagua jaji kuchukua nafasi yake kwa kipindi kilichosalia.

Majaji hao 15 lazima watoke katika nchi 15 tofauti. Mahakama kwa ujumla lazima iwakilishe aina kuu za ustaarabu na mifumo mikuu ya kisheria duniani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha