Lugha Nyingine
Rais wa Venezuela akataa "amani ya kitumwa" chini ya tishio la Marekani (2)
![]() |
| Rais wa Venezuela Nicolas Maduro akihudhuria mkutano wa hadhara mjini Caracas, mji mkuu wa Venezuela, Desemba 1, 2025. (Str/Xinhua) |
CARACAS - Venezuela haitaki "amani ya kimtumwa," Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amewaambia wafuasi wake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jumatatu mjini Caracas, Venezuela, kwa kuwa kutumwa kwa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Karibiani kumekuwa "kukiijaribu" nchi yake katika miezi kadhaa iliyopita.
"Tunataka amani, lakini tunataka amani yenye mamlaka ya nchi, amani yenye usawa, amani yenye uhuru; hatutaki amani ya watumwa au amani ya makoloni. Kamwe hatukubali kuwa koloni, na kamwe hatukubali kuwa watumwa" Maduro ametangaza, akisema kuwa "uchokozi" wa kijeshi wa Marekani wa wiki 22 unaweza kuchukuliwa kuwa ni "ugaidi wa kisaikolojia."
Maduro amesisitiza kwamba nguvu ya nchi inajengwa kwenye msingi wa ushiriki wa raia na "kutegemea nguvu kubwa ya wananchi, uelewa wao, mfumo na utaratibu wao, bunduki zao na dhamira yao ya kujenga nchi hii mbele ya ugumu wowote."
Kwa maoni yake, kuimarisha muundo huo wa jamii kutaifanya nguvu ya nchi kuwa nguvu ambayo "haiwezekani kushindwa, ya milele na ya kudumu."
Rais Maduro amesema lengo ni kulinda "amani yenye heshima" kwa kupitia kuilinda jamhuri na kulinda haki ya nchi hiyo ya kujiamulia kisiasa. Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza shinikizo kwa Venezuela kwa mkusanyiko mkubwa wa vikosi vya jeshi la majini katika eneo la Karibiani na Pasifiki, akifanya mashambulizi dhidi ya meli zilizoshukiwa kusafirisha dawa za kulevya tangu mwezi Septemba na kutoa tahadhari kali siku ya Jumamosi ya kuepuka anga ya Venezuela.
Venezuela imefuta haki za uendeshaji huduma za mashirika sita makubwa ya usafiri wa ndege ya kimataifa, na mashirika hayo yamesimamisha safari za ndege kwenda Venezuela kufuatia tahadhari kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Ndege ya Serikali Kuu ya Marekani.
Rais Maduro na serikali yake wamekanusha shutuma zote za jinai na kusema Marekani inatafuta mabadiliko ya serikali ili kudhibiti maliasili nyingi za Venezuela, ikiwa ni pamoja na mafuta.
Kwenye mawasiliano ya simu kati yao Novemba 21, Rais Trump alitoa muda wa mwisho kwa Maduro, akimtaka aondoke Venezuela, ripoti za vyombo vya habari zinasema.
Tokea mwanzoni mwa mwezi Septemba, jeshi la Marekani limefanya mashambulizi yasiyopungua 21 dhidi ya meli zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya katika eneo la Karibiani na Pasifiki, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 83.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




