Viongozi wa Uingereza, Ukraine, Ufaransa na Ujerumani wakutana London juu ya amani ya Ukraine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 09, 2025
Viongozi wa Uingereza, Ukraine, Ufaransa na Ujerumani wakutana London juu ya amani ya Ukraine
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (wa pili kushoto), Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky (wa pili kulia), Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (wa kwanza kulia) na Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz wakitoa maoni wakati walipokutana kwenye Mtaa wa No.10 wa Downing jijini London, Uingereza, Desemba 8, 2025. (Lauren Hurley/Mtaa No. 10 wa Downing /kupitia Xinhua)

LONDON - Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amekutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz mjini London jana Jumatatu kujadili amani ya Ukraine. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Uingereza baada ya mkutano huo, viongozi hao wamesisitiza hitaji la lazima la kutimiza "amani ya haki na ya kudumu ya Ukraine," ambayo inajumuisha hakikisho la usalama.

Chansela Merz alisema kabla ya mkutano huo kwamba "ana shaka na baadhi ya maelezo ambayo tunayaona kwenye nyaraka zinazotoka upande wa Marekani -- lakini tunapaswa kuyazungumzia," vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti.

Siku ya Jumamosi, wajumbe wa Marekani na Ukraine walimaliza mazungumzo ya siku tatu mjini Miami, Florida, baada ya kujadili zaidi masuala ya ardhi na uhakikisho wa usalama wa Marekani kwa Ukraine, chombo cha habari cha mtandaoni cha Marekani, Axios kiliripoti.

Rais Zelensky juzi Jumapili aliyaelezea mazungumzo ya amani na Marekani kuwa ya "kiujenzi," lakini "yasiyo rahisi."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha