Lugha Nyingine
Idadi ya waliofariki kwenye tukio la kufyatulia risasi umati wa watu katika Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Astralia yaongezeka hadi 16

Picha hii iliyopigwa Desemba 14, 2025 ikionyesha Chaneli ya Habari ya Televisheni ikitangaza tukio la kufyatulia risasi umati wa watu katika Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia. (Xinhua/Ma Ping)
SYDNEY – Taarifa ya Polisi ya mapema leo Jumatatu imesema kuwa idadi ya waliofariki katika tukio la kufyatulia risasi umati wa watu kwenye Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia lililotokea jana Jumapili usiku imeongezeka hadi kufikia watu 16, na kwamba washambuliaji ni baba na mtoto wake.
Shirika la Utangazaji la Australia (ABC) limeripoti likimnukuu Gavana wa Jimbo la New South Wales Chris Minns akisema kuwa, mshambuliaji mmoja amefariki na mwingine yuko kizuizini.
Kamishna wa Polisi wa Jimbo la New South Wales Mal Lanyon amelitangaza shambulizi hilo kuwa "tukio la kigaidi".
Mmoja wa wafyatua risasi ametajwa kuwa ni Naveed Akram kutoka Bonnyrigg kusini-magharibi mwa Sydney, ABC imeripoti, ikimnukuu afisa mwandamizi wa kusimamia utekelezaji wa sheria.
Afisa huyo, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema nyumba ya Akram katika eneo hilo la Bonnyrigg ilikuwa imezingirwa na polisi.
Televisheni ya Nine Network imeripoti kwamba watu 20 wamepigwa risasi.
Mamlaka katika jimbo hilo zimesema kuwa hakuna tishio tena lakini zimehimiza watu kuepuka eneo hilo.
Watu wengi wa jamii ya Wayahudi walikuwa wamekusanyika ufukweni kusherehekea Hanukkah, Sikukuu ya Taa ya Wayahudi, mapema siku hiyo jioni.
Gazeti la Herald Sun la Melbourne limeripoti kuwa shughuli moja ya kusherehekea Hanukkah mjini Melbourne imefutwa, na jamii ya Wayahudi katika mji huo iko katika tahadhari kubwa kufuatia tukio hilo mjini Sydney.
Ufyatuaji risasi huo ulitokea majira ya saa 12:40 jioni kwa saa za Australia wakati angalau wanaume wawili waliokuwa na bunduki zenye nguvu kubwa walifyatua risasi kwenye umati wa watu.
Tahadhari iliyotolewa na polisi muda mfupi kabla ya saa 1 jioni iliushauri umma kuepuka eneo hilo na mtu yeyote aliyekuwepo eneo la tukio (wakati huo) kujificha.
Picha na video kutoka eneo la tukio zinaonyesha watu waliokuwa wakikimbia kutoka ufukweni na silaha zilizolazwa chini.
Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese amesema katika taarifa kwamba hali katika Ufukwe wa Bondi ni "ya kushtusha," na Gavana wa jimbo la NSW Chris Minns amelielezea tukio hilo kuwa la kuhuzunisha sana.

Picha hii iliyopigwa Desemba 14, 2025 ikionyesha Chaneli ya Habari za Televisheni ikitangaza tukio la kufyatulia risasi umati wa watu katika Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia. (Xinhua/Ma Ping)

Maafisa wa polisi wakionekana karibu na eneo la shambulizi la kufyatulia risasi katika Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia, Desemba 14, 2025. (Xinhua/Ma Ping)

Maafisa wa polisi wakionekana karibu na eneo la shambulizi la kufyatulia risasi katika Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia, Desemba 14, 2025. (Xinhua/Ma Ping)

Magari ya polisi yakionekana karibu na eneo la shambulizi la kufyatulia risasi katika Ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia, Desemba 14, 2025. (Xinhua/Ma Ping)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



