Sudan na Sudan Kusini zakubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na biashara

(CRI Online) Desemba 15, 2025

Sudan na Sudan Kusini zimekubaliana jana Jumapili kuimarisha ushirikiano hasa katika sekta za nishati, mafuta, biashara, uwekezaji na masuala ya kisiasa.

Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye mkutano kati ya Mwenyekiti wa Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan Bw. Abdel Fattah Al-Burhan na ujumbe wa ngazi ya juu wa Sudan Kusini ulioongozwa na mshauri wa rais kuhusu usalama wa taifa Bw. Tut Gatluak ambaye pia aliwasilisha ujumbe wa maandishi kutoka kwa Rais Salva Kiir Mayardit kwa Bw. Al-Burhan juu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Bw. Muawiya Osman Khalid, amesema katika taarifa kwamba Bw. Al-Burhan amezihimiza taasisi husika za serikali katika ngazi za mawaziri na kiufundi kushirikiana na wenzao wa Sudan Kusini kujadili masuala yanayohusu maslahi ya pamoja ya pande hizo mbili hasa katika sekta muhimu.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha