Lugha Nyingine
China yatoa wito wa juhudi za kulinda utaratibu wa kimataifa wa baada ya Vita vya Pili vya Dunia
UMOJA WA MATAIFA - Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Fu Cong jana Jumatatu kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya uongozi kwa ajili ya amani, ametoa wito wa juhudi za kulinda utaratibu wa kimataifa wa baada ya Vita vya Pili vya Dunia (WWII).
Balozi Fu amesema umilitalizm (militarism) na ufashisti hapo awali vilileta majanga yasiyo na kifani kwa binadamu na kwamba kauli na vitendo vyovyote visivyo sahihi vya kusafisha au kupindua historia ya uvamizi vinapinga msingi wa dhamiri ya binadamu na kuharibu amani iliyopatikana kwa ngumu.
"Lazima tushikilie mtazamo sahihi kuhusu historia ya Vita vya Pili vya Dunia, kulinda matokeo ya ushindi ya Vita vya Pili vya Dunia, na kulinda utaratibu wa kimataifa wa baada ya vita." Amesema.
"Lazima tufuate madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa, kushikilia usawa wa mamlaka wa nchi zote, bila kujali ni kubwa au ndogo, kupinga maamuzi ya upande mmoja, umwamba, na siasa za kutumia nguvu, tusukume mbele kuufanya uhusiano wa kimataifa uwe wa kidemokrasia, na kuongeza uwakilishi na sauti za nchi zinazoendelea katika masuala ya kimataifa" ameongeza.
Balozi Fu ametoa wito wa kujitolea katika utatuzi wa kisiasa kama njia bora ya kufikia amani, akisema kwamba amani inapatikana si kupitia nguvu, bali kupitia mazungumzo na kwamba mgogoro wowote utamalizwa kwenye meza ya mazungumzo.
"Nchi kubwa, haswa, zinapaswa kuonyesha dhamira na kubeba jukumu la kiujenzi, kujiepusha kuchukua viwango viwili au kulazimisha nia zao kwa wengine, na zaidi ya hayo, kuepuka kuchochea migogoro kwa ajili ya maslahi finyu ya kibinafsi," ameongeza.
Balozi Fu ametoa wito wa juhudi za kushikilia mfumo wa pande nyingi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda amani.
"Utamaduni wa jadi wa China kwa muda mrefu umeshikilia maadili ya amani kama jambo muhimu na kuishi pamoja kwa masikilizano. Kwa maelfu ya miaka, amani imekuwa katika damu ya taifa la China na DNA ya watu wa China. China itaendelea kushirikiana na nchi zote ili kuhimiza kikamilifu ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja na kutoa mchango katika harakati ya amani na maendeleo duniani" amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



