UN yasema Raia 104 wameuawa katika mashambulizi ya droni huko Kordofan nchini Sudan tangu Desemba 4

(CRI Online) Desemba 17, 2025

Umoja wa Mataifa umesema angalau raia 104 wameuawa katika mashambulizi ya droni huko Kordofan nchini Sudan tangu tarehe 4 Desemba na kuelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa uhasama kati ya pande zinazopigana nchini humo.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Bw. Volker Turk amesema kwenye taarifa yake jana Jumanne kuwa katika shambulizi moja, droni ilishambulia shule ya chekechea na hospitali huko Kalogi katika Jimbo la Kordofan Kusini na kusababisha vifo vya raia wasiopungua 89, wakiwemo wanawake wanane na watoto 43.

Bw. Turk amezihimiza pande zote za mgogoro huo, pamoja na mataifa yenye ushawishi, kuhimiza usimamishaji wa vita wa mara moja na kuzuia ukatili zaidi.

Pia amelaani mauaji ya walinzi sita wa amani wa Umoja wa Mataifa katika mashambulizi ya droni dhidi ya kambi ya Umoja wa Mataifa huko Kadugli, Kordofan Kusini, akionya kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha