Japan yaendelea kuwa na msimamo wenye utata kuhusu suala la Taiwan na kuwapotosha umma: Msemaji wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 17, 2025

BEIJING - Kwa kuzingatia mfululizo wa kauli, Japan bado inaendelea kuwa na msimamo wenye utata na kwa makusudi imeacha masuala muhimu bila kutatuliwa juu ya suala la Taiwan, kwa lengo la kupotosha umma na kukwepa wajibu wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Guo Jiakun amesema.

"China inapinga vikali vitendo kama hivyo," Msemaji Guo amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne.

Akijibu swali husika kuhusu taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Toshimitsu Motegi kuhusu swala la Taiwan kwenye kikao katika Baraza la Madiwani la Japan, Guo amesema upande wa Japan haukusisitiza kifungu muhimu cha Taarifa ya Pamoja kati ya China na Japan ambacho kinasema "Serikali ya Japan inatambua Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuwa ni Serikali pekee halali ya China" na "Taiwan ni sehemu isiyotengeka ya Jamhuri ya Watu wa China."

Msemaji huyu aliendelea kueleza kwamba upande wa Japan wakati ukirejelea Azimio la Cairo ulitaja tu "Manchuria, Formosa, na visiwa vya Pescadore" na kwa makusudi uliweka kando taarifa muhimu kwamba ni "ardhi ambazo Japan imeiba kutoka kwa Wachina."

"Upande wa Japan pia umelinganisha Taarifa ya Pamoja kati ya China na Japan na kile kinachoitwa Mkataba wa San Francisco, ukikiuka ahadi ulizotoa na misingi ya sheria za kimataifa, ukijaribu kuhuisha uongo kwamba hadhi ya Taiwan "haijulikani" na kuingilia mambo ya ndani ya China," amesema Guo.

Guo pia amerejelea kauli za maafisa mbalimbali waandamizi wa Japan na taarifa katika nyaraka husika kuwa ni ukweli wa kihistoria unaozungumzia msimamo wa Japan kuhusu suala la Taiwan.

"Tunausihi tena upande wa Japan kufuata moyo wa nyaraka nne za kisiasa kati ya China na Japan, kujitafakari kwa kina na kurekebisha makosa yake na kufuta kauli zenye makosa zilizotolewa na Waziri Mkuu Sanae Takaichi," Guo ameongeza. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha