Lugha Nyingine
Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Cape Coast cha Ghana yaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake
ACCRA - Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Cape Coast Jumatatu iliadhimisha miaka 10 tangu kuanza rasmi kutoa elimu ya lugha na utamaduni wa Kichina katika mji wa kihistoria wa Cape Coast, mji mkuu wa Mkoa wa Kati wa Ghana.
Hafla ya maadhimisho hayo, yenye kaulimbiu ya "Muongo mmoja wa mawasiliano ya kitamaduni na ubora katika elimu ya lugha ya Kichina," iliambatana na maonyesho mbalimbali ya utamaduni wa Kichina yaliyofanywa na wanafunzi wa shule za msingi na wa vyuo vikuu.
“Taasisi ya Confucius, ambayo ilianza kama mpango mdogo, imekua na kuwa taasisi yenye hadhi na umuhimu mkubwa,” amesema Denis Worlanyo Aheto, kaimu makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Cape Coast.
Amesema kwamba Taasisi ya Confucius imewapa mafunzo wanafunzi wa Ghana katika lugha na utamaduni wa Kichina ambao wanatoa mchango katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
"Tangu kuanzishwa kwake, Taasisi ya Confucius imekuwa ikitoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 11,000 kila mwaka. Taasisi hiyo inaendelea kuwa nguvu ya uongozi katika kukuza ujuzi wa lugha nyingi, kuelewana kunakovuka tamaduni mbalimbali, na sifa za uraia duniani ambazo zinahitajika katika dunia ya leo iliyo na muunganisho mkubwa," ameongeza.
Ou Yamei, Mkurugenzi Mchina wa Taasisi ya Confucius, amesema kwamba Taasisi ya Confucius imejitolea kukuza wataalamu wa lugha ya Kichina kwa ajili ya Ghana na nchi jirani, na imetoa mchango kwenye elimu ya lugha ya Kichina nchini Ghana.
Katika hafla hiyo, jumla ya wanafunzi 74 kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu waliofanya vizuri katika masomo ya lugha ya Kichina walipewa Tuzo za Balozi wa China za 2025.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



