Shughuli za kibinadamu zasimamishwa katika miji miwili baada ya mapambano makali kuibuka Kivu Kusini nchini DRC

(CRI Online) Desemba 17, 2025

Umoja wa Mataifa umesema jana Jumanne kuwa Kufuatia mapambano kutokea katika sehemu kadhaa za Jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), shughuli zote za kibinadamu zimeendelea kusimamishwa katika miji ya Fizi na Baraka.

Akinukuu ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) kwenye mkutano na waandishi wa habari wa kila siku, naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Farhan Haq amesema vurugu zilizotokea hivi karibuni zimezua hofu kwa raia, na washirika wa Umoja wa Mataifa pia wameripoti matukio ya uporaji wa mali yaliyofanywa na watu wenye silaha.

Mamlaka nchini DRC zimekadiria kuwa tangu Desemba 8, watu takriban 110,000 wamekimbilia sehemu nyingine za Kivu Kaskazini, huku wengine wakivuka mpaka na kuingia Burundi. Pia kuna ripoti kuhusu watu wanaoendelea na safari ya kuelekea Tanzania.

Amesema OCHA inaendelea kushirikiana na pande zote kurahisisha usafiri salama wa timu za misaada ya kibinadamu na kurejesha operesheni za misaada.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha