Lugha Nyingine
Kupaza sauti kwa vipaji vya Afrika
![]() |
| Shindano la muziki la Imba kwa Afrika (Sing for Africa) likifanya mchujo wa wazi wa washiriki katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, na kuvutia washiriki zaidi ya 500. (China Daily) |
Kituo cha Televisheni ya Satalaiti cha Hunan, China kina historia ndefu ya kuandaa vipindi maarufu vya vipaji vinavyolenga jinsia mahususi, kama vile Super Girls (2004), Super Boy (2007), Riding Wind, na Call Me by Fire. Kikijenga juu ya muundo huo uliofanikiwa, chaneli ya kimataifa ya kituo hicho cha televisheni sasa inapanua ufikiaji wake hadi Afrika kupitia uzinduzi wa shindano jipya la vipaji, Imba kwa Afrika (Sing for Africa).
Shindano hilo la vipaji linaloshirikisha wanaume pekee limevutia kwa kasi, likiwakusanya zaidi ya washiriki 500 kwenye mchujo wa wazi wa kwanza hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya.
Miongoni mwa washiriki ni Shimon Kinyanjui mwenye umri wa miaka 22, mtayarishaji wa maudhui na mwanamitindo anayejulikana kwa video za vichekesho bunifu na video za kuigilizia sauti kwa mienendo sawa ya midomo (lip-synch) kwenye Instagram na TikTok.
Akitiwa moyo na wafuatiliaji wake mtandaoni kushiriki mchujo huo wa kipindi cha maonyesho ya vipaji, amesema, "Kujiunga na kipindi hiki ni jambo ambalo sikuwahi kufikiria ningelifanya, lakini hadi sasa, nasema, wow, ni jambo la kufurahisha na la kushangaza."
"Ninapozungumzia malengo ya muda mrefu, namaanisha fursa kubwa za Billboard, kufanya kazi na watayarishaji, kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine, na pia kuihudumia familia yangu kwa maisha bora zaidi. Nataka kuwa kaka ambaye familia yangu inaweza kumtegemea,” amesema.
Allan Bosire, baba mlezi pekee wa mtoto wa kiume wa miaka 2, pia anasukumwa na dhamira yake kwa familia kushiriki kwenye shindano hilo.
Akiwa ni mpiga ala aliyejifunza mwenyewe, anaona fursa hiyo ni muhimu katika kujenga taaluma endelevu ya muziki, ambayo si tu inatimiza ndoto zake mwenyewe lakini pia inayomtia moyo mwanawe.
"Ni shindano kubwa la kwanza ambalo nimewahi kushiriki, na kwa kweli, ninajitahidi kujifunza hatua kwa hatua. Lakini hadi sasa, mambo yanaendelea vizuri," Bosire anasema.
Msimu huo wa Imba kwa Afrika (Sing for Africa) umepangwa katika hatua tatu: mchujo wa wazi, raundi za mtoano, na fainali kuu.
Mbali na zawadi ya juu ya shilingi milioni 1 za Kenya (Dola za Marekani 7,760), mshindi wa mwisho wa shindano hilo pia atapata fursa ya kufanya maonyesho jukwaani nchini China, kusaini mkataba wa kurekodi, na kushirikiana na wanamuziki mashuhuri wa China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




