Sherehe za Mwaka Mpya wa Kikabila nchini China zavutia wageni wa kimataifa (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 24, 2025
Sherehe za Mwaka Mpya wa Kikabila nchini China zavutia wageni wa kimataifa
(Picha/VCG)

GUIYANG - Kwa midundo ya ala ya lusheng na harufu nzuri ya keki za mchele zenye kunata, Kijiji cha Kabila la Wadong cha Zhaoxing katika Wilaya ya Liping, Eneo Linalojiendesha la Makabila ya Wamiao na Wadong la Qiandongnan, Mkoa wa Guizhou, Kusini Magharibi mwa China kimesherehekea Mwaka Mpya wa Jadi wa Kabila la Wadong mwishoni mwa wiki, tukio ambalo limekuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka duniani kote.

Kikijulikana kama moja ya vijiji vikubwa vya kabila la Wadong nchini China, Kijiji cha Zhaoxing katika Wilaya ya Liping huandaa shughuli za kipekee za kitamaduni kila mwaka, ikiwa ni pamoja na kukaanga keki za jadi za kabila la Wadong, kuimba wimbo mkuu wa kabila la Wadong, kuandaa magwaride makubwa ya kikabila, mashindano ya muziki wa lusheng, na sherehe za moto.

Tamasha hilo lenye uhai na shamrashamra limevutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani, na kuunda mazingira ya shangwe na furaha.

Konstantin Pokazachenko, mtalii kutoka Moscow, Russia, aliwasili kwa treni ya mwendokasi kutoka Guilin, eneo maarufu la utalii katika Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi. Yeye na marafiki zake wamekaa katika kijiji hicho kwa siku mbili. Wakati huu, walitembelea majengo mengi ya kale, kushuhudia gwaride kubwa na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za jadi.

"Nimeshawahi kuona maonyesho ya nyimbo na ngoma za makabila ya China hapo awali, lakini sherehe hiyo ya Mwaka Mpya wa Kabila la Wadong limeshirikisha washiriki wengi zaidi na maonyesho mbalimbali. Kuishuhudia moja kwa moja ni jambo la kuvutia sana," amesema.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uhamiaji ya China (NIA), watalii kutoka nchi 76 sasa wanaweza kuingia China bila visa, huku sera ya kusamehe visa kwa wasafiri wanaoingia China kwa kuunganisha ndege kwenda nchi nyingine ikipanuliwa hadi nchi 55.

Takwimu za NIA zinaonyesha kuwa kuingia bila visa kulichangia zaidi ya watalii milioni 7 wa kigeni katika robo ya tatu ya mwaka huu, sawa na asilimia 72.2 ya watalii wote wanaoingia China na kuashiria ongezeko la asilimia 48.3 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Kutokana na sera hiyo ya kuingia bila visa, watalii wengi zaidi wa kimataifa wanachagua maeneo ya mbali ya milimani kusini-magharibi mwa China kama vituo vyao vya utalii, na kuongeza hali ya kimataifa katika eneo hilo.

Chloe Bertrand, anayefanya kazi katika Mkoa wa Guangdong, alitembelea kijiji hicho kwa mara ya kwanza akiwa na wazazi wake na dada yake, ambao walisafiri kwa ndege hadi China kwa ajili ya likizo ya Krismasi.

"Tulichagua maeneo ya vijijini ya Guizhou kama kituo chetu cha mwisho cha safari yetu nchini China ili kushuhudia mila za kikabila za wenyeji," amesema, akiongeza kuwa Guizhou yenye milima pia ni eneo bora kwa shughuli za kupanda milima.

Hadi sasa, takriban watalii 10,000 wa kigeni wameitembelea kijiji hicho, takwimu zinaonyesha.

“Kupitia kuandaa shughuli kama vile sherehe za Mwaka Mpya wa Jadi wa Kabila Wadong na mashindano ya kwaya ngazi ya kijiji, mamlaka za mitaa zimeanzisha miradi ya kipekee ya utalii wa kitamaduni wa kikabila ambayo imestawisha utalii wa vijijini kwa uzoefu mbalimbali wa kitamaduni,” amesema Lu Weimin, katibu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa kijiji hicho.

Lu ameongeza kuwa, Kijiji hicho sasa kina zaidi ya hoteli, nyumba za wageni na migahawa 400, na kutoa ajira na fursa za ujasiriamali kwa wanakijiji zaidi ya 2,000.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha