Ambapo maji safi hutiririka, magonjwa hupungua: Jitihada za China za kudhibiti kichocho zaokoa maisha Zanzibar (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 04, 2026
Ambapo maji safi hutiririka, magonjwa hupungua: Jitihada za China za kudhibiti kichocho zaokoa maisha Zanzibar
Wang Wei, kiongozi wa timu ya wataalamu Wachina akielezea kinga ya kichocho kwa wakazi wa Kisiwa cha Pemba, Zanzibar, Tanzania, Januari 1, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

ZANZIBAR - Kwa kufungua bomba kwa taratibu, maji safi yanatoka -- jambo ambalo wakazi wa Kijiji cha Chaani, katika Kisiwa cha Unguja, Zanzibar, Tanzania kwa muda mrefu walikuwa wameamini haliwezekani.

Kilichoko katika Mkoa wa Kaskazini wa Zanzibar kwenye Kisiwa cha Unguja, Kijiji cha Chaani kimekabiliwa kwa miongo kadhaa na uhaba wa vyanzo salama vya maji. Hali hiyo ilianza kubadilika mwaka 2025.

"Kwa miaka mingi, maji yalikuwa tatizo letu kubwa," amesema Haji Makame Omari mwenye umri wa miaka 53, baba wa watoto wanane na mkazi wa Chaani.

"Tulichota maji kutoka kwenye mito, na hapo ndipo tulipoambukizwa kichocho. Sasa hatuendi huko tena. Tunajihisi salama," amesema, akipongeza mradi wa kudhibiti kichocho unaosaidiwa na China ambao unatekelezwa kwa pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) na serikali ya Zanzibar nchini Tanzania.

Katika kijiji hicho cha Chaani, ambacho ni moja ya wanufaika wa mradi huo, maji safi sasa hutiririka asubuhi, adhuhuri, na usiku, mabadiliko rahisi yaliyobadilisha maisha ya kila siku na kusaidia kupunguza moja ya magonjwa sugu zaidi katika eneo hilo, kichocho.

Kupitia kuunganisha mifumo ya maji salama na matibabu ya ugonjwa, udhibiti wa konokono na elimu ya afya, mradi huo umepunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi huku ukiboresha maisha ya wakazi.

Kichocho ni ugonjwa unaoambukizwa na vimelelea vilivyoko kwenye maji, kwa muda mrefu umekuwa mzigo kwa Zanzibar, hasa maeneo ya vijijini, ambako wakazi walitegemea mito na visima vilivyochafuliwa, wakijiweka katika hatari ya kuambukizwa. Akina mama kama Mwanaisha Abdallah mwenye umri wa miaka 30, ambaye pia ni mwanakijiji wa Chaani, wamekumbuka safari za mara kwa mara hospitalini kwa watoto wao kutokana na magonjwa yanayohusiana na maji.

Kwa wanawake, ambao kwa muda mrefu walibeba mzigo mkubwa wa kuchota maji na kutunza watoto, mabadiliko hayo yamekuwa ya kimageuzi.

"Hapo awali, tulihangaika sana. Sasa nachukua tu ndoo yangu, kutembea umbali mfupi, kisha narudi. Ninaweza kulima mboga za majani, kufuga kuku, na kufua nguo kwa urahisi. Furaha katika familia yangu imeongezeka." Abdallah amesema.

Nyuma ya mabadiliko hayo kuna juhudi ya ushirikiano wa muongo mmoja.

Kwa mujibu wa Wang Wei, kiongozi wa timu ya wataalamu Wachina yenye watu watano ambao pia ni profesa katika Taasisi ya Magonjwa ya Vimelea ya Jiangsu ya China, ushirikiano ulianza baada ya Zanzibar kutafuta msaada wa kimataifa mwaka 2014, wakati kiwango cha maambukizi ya kichocho kilikuwa juu licha ya juhudi za awali za udhibiti.

"Uzoefu wa China katika kudhibiti kichocho tayari ulikuwa umethibitishwa kuwa mzuri na unaoweza kupanuliwa katika nchi nyingine. Juu ya msingi wa ahadi za pamoja, China, WHO, na serikali ya Zanzibar walitia saini makubaliano ya maelewano, na mradi huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2016." Wang amesema.

Kwa mujibu wa takwimu za mradi huo, Awamu ya kwanza ya mradi huo, iliyotekelezwa katika Kisiwa cha Pemba kuanzia 2017 hadi 2020, ilipunguza viwango vya maambukizi katika maeneo ya kielelezo kutoka asilimia 8.92 hadi asilimia 0.64, ikikidhi vigezo vya WHO kwa ajili ya kukiondoa kichocho kuwa tatizo la afya ya umma. Awamu ya pili, iliyozinduliwa mwaka 2023, ilipanua wigo wa huduma hadi Kisiwa cha Unguja.

Matokeo yamekuwa ya kushangaza. Uchunguzi wa msingi ulionyesha kiwango cha maambukizi cha asilimia takriban 1.23. Baada ya miaka miwili na nusu, takwimu mpya zinaonyesha kushuka hadi asilimia 0.15 tu, chini ya kiwango cha WHO cha asilimia 1.

Ubunifu muhimu katika Awamu ya pili ni ujenzi wa mifumo ya maji salama. Miradi mitano -- minne katika Kisiwa cha Pemba na mmoja katika Kisiwa cha Unguja -- sasa inahudumia watu takriban 30,000 kwa jumla.

"Huu ni mradi halisi wa maisha. Si tu kwamba unadhibiti ugonjwa bali pia unaboresha maisha ya kila siku." Wang amesema.

Rashid Kassim Juma, mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Maji, Nishati, na Madini ya Zanzibar, ameuelezea mpango huo kuwa ni "msaada mkubwa kutoka China."

Zaidi ya miundombinu, mradi huo umejikita katika uendelevu. Hospitali za jamii na watu wa kujitolea wamepewa mafunzo, vituo vya elimu ya afya na shule za kielelezo vimeanzishwa, na mifumo ya ufuatiliaji imejumuishwa hatua kwa hatua kwenye mifumo ya taarifa za afya ya Zanzibar.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha