Lugha Nyingine
Mauzo ya bidhaa zisizotozwa ushuru ya likizo ya Mwaka Mpya yaongezeka kwa asilimia 128.9 katika Hainan, China
![]() |
| Mteja akichagua bidhaa kwenye duka la bidhaa zisizotozwa ushuru mjini Haikou, Mkoani Hainan, kusini mwa China, Januari 1, 2026. (Xinhua/Yang Guanyu) |
HAIKOU – Idara ya Forodha ya Haikou imesema kwamba ununuzi wa bidhaa zisizotozwa ushuru katika mkoa wa kisiwa cha mapumziko cha Hainan, kusini mwa China umeanza kwa kasi wakati wa likizo ya Mwaka Mpya wa 2026, huku mauzo bidhaa zisizotozwa ushuru kwenye eneo hilo yakifikia yuan milioni 712 (sawa na dola za Marekani takribani milioni 101.3) kuanzia Januari 1 hadi 3, ongezeko la asilimia 128.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
"Idara ya Forodha imerekodi mauzo ya bidhaa 442,000 zisizotozwa ushuru katika kipindi cha likizo ya siku tatu, ongezeko la asilimia 52.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, huku idadi ya wanunuzi ikiongezeka kwa asilimia 60.6 ikilinganishwa na mwaka jana hadi kufikia 83,500," idara hiyo ya forodha imesema jana Jumapili.
Imeeleza kuwa, maduka makubwa ya bidhaa zisizotozwa ushuru yalitoa ofa mbalimbali ili kuchochea matumizi, ikiwemo mapunguzo ya bei na vocha, na mengi yalitoa pia maonyesho ya burudani na mabasi ya usafiri wa bila malipo ili kuvutia watumiaji.
Kwa mujibu wa idara hiyo ya forodha, ukuaji huo wa haraka unafuatia utekelezaji wa sera mpya ya kutotoza ushuru iliyoanza Novemba 2025, ambayo ilipanua wigo wa bidhaa zinazostahiki. Bidhaa mpya maarufu ni pamoja na droni ndogo na gitaa za kielektroniki, huku bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kama vile fomula ya watoto wachanga na nepi za watoto zikionyesha mahitaji makubwa ya wakazi.
Kwa sasa, wasafiri wanaotembelea kisiwa hicho wanaweza kufurahia kikomo cha ununuzi wa bidhaa zisizotozwa ushuru cha yuan 100,000 kwa kila mtu kwa mwaka. Mkoa huo umeripoti mauzo makubwa ya bidhaa zisizotozwa ushuru kwenye eneo hilo katika miaka michache iliyopita tangu kuongeza kikomo cha kila mwaka cha ununuzi wa bidhaa zisizotozwa ushuru kutoka yuan 30,000 hadi yuan 100,000 kwa kila mtu Julai 1, 2020.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




