Lugha Nyingine
Kaburi la Enzi ya Tang lenye mabaki liyotengenezwa kwa ustadi wa hali ya juu lafukuliwa mjini Xi'an, China
XI'AN - Wanaakiolojia katika Mkoa wa Shaanxi, kaskazini magharibi mwa China wamegundua kaburi la Enzi ya Tang (miaka ya 618-907), na kufukua mkusanyiko wa kauri, vyombo vya shaba, na vitu vya dhahabu na fedha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Akademia ya Akiolojia ya Shaanxi siku ya Jumanne.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, ufukuaji huo ulifanyika kati ya Januari 2022 na Aprili 2024 katika Kijiji cha Jiali cha Eneo la Chang'an mjini Xi'an, mji mkuu wa mkoa huo, kabla ya mradi wa ukarabati wa eneo hilo. Miongoni mwa makaburi ya kale katika eneo hilo la mradi, moja lililowekewa alama ya M228 limetambuliwa kuwa ni kaburi la Ma Sanniang, mke wa Dong Shunxian, afisa wa kijeshi katika Enzi ya Tang, aliyezikwa mwaka 698 AD.
Jumla ya vitu 19 au seti za mazishi vimepatikana, vikiwemo vyombo vya udongo, shaba, chuma, dhahabu na fedha, pamoja na vitu vya mawe. Hasa, baadhi ya vitu vya dhahabu na fedha vimeonyesha kiwango cha juu cha ufundi.
Kwa mujibu wa Shi Sheng, mfanyakazi wa Akademia ya Akiolojia ya Shaanxi, sehemu kubwa ya vitu vya dhahabu na fedha vilikuwa mapambo ya nywele ya wanawake au vyombo vya kuhifadhia.
Amesema jagi la fedha na kikombe cha silva chenye kishina cha kushikia vimepambwa hasa kwa michoro ya mizabibu, mtindo ulioathimiwa na maeneo ya Magharibi, ikionesha mwingiliano mkubwa wa kiutamaduni kati ya maeneo ya tambarare ya kati ya China na Maeneo ya Magharibi katika kipindi hicho.
“Vitu hivi vya dhahabu na fedha vina thamani kubwa ya utafiti, na vinatoa ushahidi mpya wa kimali kwa ajili ya kuchunguza mawasiliano ya kiutamaduni na kibiashara kati ya China na ustaarabu mwingine mbalimbali wakati wa kilele cha Enzi ya Tang,” Shi ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




