Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya China yafikia kiwango kipya cha juu, ikiongezeka kwa asilimia 3.8 mwaka 2025 (3)
![]() |
| Picha hii iliyopigwa Januari 14, 2026 ikionyesha mandhari ya Gati la Makontena la Longtan kwenye Bandari ya Nanjing, Mkoani Jiangsu, mashariki mwa China. (Picha na Xin Yi/Xinhua) |
BEIJING - Takwimu zilizotolewa na Mamlaka Kuu ya Forodha ya China Jumatano zinaonyesha kuwa biashara ya nje ya China iliongezeka kwa asilimia 3.8 mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia wa 2024 ambapo thamani ya biashara ya nje ya China ilifikia yuan trilioni 45.47 (takribani dola za Marekani trilioni 6.48).
Huu ni mwaka wa tisa mfululizo ambapo biashara ya nje ya China imeendelea kukua tangu mwaka 2017.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa mauzo ya nje ya bidhaa ya China yaliongezeka kwa asilimia 6.1 ikilinganishwa na mwaka 2024, na kufikia yuan trilioni 26.99 mwaka 2025. Wakati huohuo uagizaji bidhaa kutoka nje ulifikia rekodi ya yuan trilioni 18.48, ukiwa na ukuaji wa asilimia 0.5 ikilinganishwa na mwaka 2024, hali iliyoimarisha nafasi ya China kama soko la pili kwa ukubwa duniani la uagizaji bidhaa nje ya nchi kwa miaka 17 mfululizo.
Katika kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025), thamani ya jumla ya biashara ya uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya China ilizidi yuan trilioni 200, sawa na ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na kipindi cha Mpango wa 13 wa Miaka Mitano, huku wastani wa ukuaji wa kila mwaka ukiwa asilimia 7.1.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari wa serikali uliofanyika Beijing jana Jumatano, Wang Jun, naibu mkuu wa Mamlaka Kuu ya Forodha ya China, amesema kwamba mafanikio ya biashara ya nje ya China ni "makubwa na yamepatikana kwa juhudi kubwa", licha ya changamoto za uchumi duniani.
Wang amesema kuwa ukuaji thabiti wa biashara ya nje ya China umechochewa na mambo matatu makuu: Sera za China za kuimarisha utulivu wa biashara ya nje, kuendelea kuongezeka kwa mahitaji ya uagizaji bidhaa nje kutoka soko lake kubwa la ndani, na mfumo wa kisasa wa viwanda unaoendelea kuendana na mahitaji yanayobadilika kila wakati ya soko ya ng'ambo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




