Lugha Nyingine
Pato la Taifa la China laongezeka kwa asilimia 5 mwaka 2025, likifikia lengo la mwaka

Mkuu wa Idara ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) Kang Yi (Katikati), na msemaji na mchumi mkuu wa NBS ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Takwimu Jumuishi ya NBS Fu Linghui (Kulia), wakihudhuria mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China (SCIO) kuhusu hali ya uchumi wa China mwaka 2025, mjini Beijing, mji mkuu wa China, Januari 19, 2026. (Xinhua/Shan Yuqi)
BEIJING - Pato la Taifa la China (GDP) lilikua kwa asilimia 5 katika mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024 wakati kama huo, na kufikia lengo la mwaka la ukuaji wa karibu asilimia 5, kwa mujibu wa takwimu rasmi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) zilizotolewa jana Jumatatu. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Pato la Taifa la China lilifikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa cha yuan trilioni 140.1879 (takribani dola za Marekani trilioni 20.01) mwaka jana.
NBS imesema katika robo ya nne ya mwaka 2025, uchumi wa China uliongezeka kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na mwaka 2024 wakati kama huo, na kukua kwa asilimia 1.2 ikilinganishwa na robo iliyotangulia.
"Licha ya mazingira tata ya ndani na nje, uchumi uliendelea kusonga mbele chini ya shinikizo, na kufikia maendeleo mapya katika maendeleo yenye sifa bora," NBS imeeleza.
Imeongeza kuwa malengo na majukumu makuu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii yalifikiwa kikamilifu mwaka 2025, na hivyo kukifikisha kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025) kwenye hitimisho lenye mafanikio.
"Katika kukabili mabadiliko ya ghafla katika mazingira ya nje na kuongezeka kwa mambo magumu na changamoto za ndani, China ilitekeleza sera za jumla zilizo makini zaidi na zenye ufanisi, hatua ambazo zilisaidia kukabiliana na athari mbaya na mishtuko ya nje na kuimarisha msingi wa maendeleo katika mazingira yenye changamoto," Kang Yi, Mkuu wa NBS, amesema katika mkutano na waandishi wa habari.
Ameongeza kuwa kwa nchi yenye uchumi mkubwa sana kama China, kufikia maendeleo thabiti ya namna hiyo si jambo rahisi, hasa katika mazingira yanayokabiliwa na hatari na changamoto zinazochanganyika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



