Waziri Mkuu wa Japan Takaichi kulivunja baraza la chini la bunge Ijumaa kwa ajili ya uchaguzi wa Februari 8

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 20, 2026

TOKYO - Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi ametangaza mpango wake wa kulivunja Baraza la Chini la Bunge la nchi hiyo Ijumaa wiki hii Januari 23 ili kufanya uchaguzi mkuu Tarehe 8 Februari kabla ya mpango uliowekwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumatatu, Takaichi amesema atalivunja baraza hilo la chini la bunge la taifa lenye wabunge 465 Ijumaa wiki hii, ambayo ni siku ya kufungua mkutano wa kawaida wa bunge hilo wa mwaka huu.

“Upigaji kura utafanyika Februari 8, huku kampeni rasmi zikianza Januari 27,” ameongeza.

Uchaguzi huo ni uchaguzi wa kwanza tangu Takaichi aingie madarakani Oktoba 21, hivi sasa bado umebakia miaka zaidi ya miwili kwa muda wa madaraka ya baraza hilo la chini.

Wiki iliyopita, Takaichi alielezea nia yake ya kulivunja baraza la chini muhimu la bunge kwa wanachama waandamizi kutoka chama chake tawala cha Liberal Democratic (LDP) na chama mshirika wake wa muungano cha Japan Innovation Party.

Ili kupambana na kambi tawala, Chama cha Demokrasia cha Kikatiba cha Japan na chama cha Komeito, mshirika wa zamani wa muda mrefu wa LDP, vilikubaliana Alhamisi wiki iliyopita kuunda Muungano wa Mageuzi wa Mrengo wa Kati, ambao utakuwa nguvu kubwa zaidi ya upinzani katika uchaguzi ujao.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha