Jeshi la DRC lachukua tena udhibiti wa Mji wa Uvira baada ya M23 kuondoka

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 21, 2026

KINSHASA - Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vimesema katika taarifa ya Jumatatu jioni kwamba vimechukua tena udhibiti wa Uvira, mji wa kimkakati katika jimbo la mashariki la Kivu Kusini ambao ulikuwa umekaliwa na waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23).

Kwenye taarifa hiyo, FARDC imesema uchukuaji tena huo wa udhibiti wa Uvira umetokea siku ya Jumapili, baada ya wapiganaji wa M23 kuondoka.

Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Mak Hazukay Mongba, msemaji wa muda wa FARDC, imewashutumu waasi hao kwa kufanya "uporaji mfululizo uliopangwa" kabla ya kuondoka katika mji huo. Imesema raia takriban 20 wanaoshukiwa kuhusika na uporaji huo wamekamatwa na watapelekwa kwenye mikono ya sheria.

"Vikosi vya FARDC vinaendelea kupeleka askari wake huko Uvira na maeneo ya pembezoni mwake ili kuimarisha nafasi zao na kulinda watu na mali zao," jeshi hilo limesema.

Katika taarifa nyingine iliyotolewa siku hiyo ya Jumatatu, serikali ya DRC imesema imeanza kutekeleza mpango wa kurejesha mamlaka ya nchi hatua kwa hatua katika mji huo wa Uvira na maeneo ya pembezoni mwake katika sehemu ya mashariki ya nchi hiyo.

Siku ya Jumamosi, M23 ilisema itaondoa kikamilifu uwepo wake uliobaki kutoka Uvira. Uvira ni mji wa kimkakati ulioko kando ya Ziwa Tanganyika, M23 ilijidai kuwa iliwahi kuuteka mwezi Desemba 2025.

Kwenye taarifa yake, msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka alisema hatua ya kuondoka kwa M23 ni "uamuzi mgumu" na alisema kundi hilo liko katika kuondoa kile lilichokieleza kuwa ni "kitengo cha uangalizi na ufuatiliaji."

Kanyuka alisema kundi hilo linaiweka Uvira "chini ya wajibu kamili wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa." M23 ilisema ilikuwa ikiondoka ni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa juhudi za amani katika eneo hilo, lakini haikudokeza idadi gani hasa ya wapiganaji waliohusika.

Kundi hilo la waasi pia lilisema lilikuwa limeuomba ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ulioko nchini humo, unaojulikana kwa jina la MONUSCO, utafuata jukumu lake la kulinda raia katika mji huo wa Uvira . Hata hivyo, MONUSCO haikutoa taarifa kuhusu ombi hilo.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha