Mapigano yanayoongezeka katika Jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan yanasa raia na kutatiza ufikiaji wa misaada

(CRI Online) Januari 22, 2026

Mapigano yanayoongezeka katika Jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan yamenasa raia na kuzuia ufikiaji wa misaada ya kibinadamu, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema jana Jumatano.

OCHA imeeleza wasiwasi kuhusu hali mbaya ya maelfu ya raia ambao wametengwa kutoka kwenye misaada katika jimbo hilo la Darfur Kaskazini, huku washirika wa misaada jimboni humo wakiripoti kuwa familia karibu 2,000 zimenaswa katika mabonde ya Wadi Qardi na Um Saada kwenye maeneo ya Karnoi na Um Baru.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linakadiria kuwa, watu karibu 3,000 wamekimbia makazi yao kati ya Januari 15 na 19 kutoka miji ya Kadugli na Dilling katika Jimbo la Darfur Kusini, huku wengine wakikimbilia Jimbo la White Nile.

OCHA imesema, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaongeza msaada, ikiwemo viwango vya mgao wa chakula, mahema, magodoro, na maji, vilevile huduma za usafi na afya, lakini bado kuna pengo kubwa kutokana na uhaba wa fedha.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha