China yawatunuku medali wanaanga watatu wa chombo cha Shenzhou-20

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 22, 2026

Wanaanga watatu Chen Dong (katikati), Chen Zhongrui (kulia) na Wang Jie kutoka misheni ya Shenzhou-20 ya China wakipiga saluti kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, mji mkuu wa China, Januari 16, 2026. (Xinhua/Li Minggang)

Wanaanga watatu Chen Dong (katikati), Chen Zhongrui (kulia) na Wang Jie kutoka misheni ya Shenzhou-20 ya China wakipiga saluti kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, mji mkuu wa China, Januari 16, 2026. (Xinhua/Li Minggang)

BEIJING - Wanaanga watatu wa China Chen Dong, Chen Zhongrui na Wang Jie walioshiriki kwenye misheni ya safari ya anga ya juu ya chombo cha Shenzhou-20, walipewa medali jana Jumatano kwa mchango wao katika mpango wa anga ya juu wa China.

Chen Dong amekabidhiwa medali ya daraja la kwanza ya mafanikio ya anga ya juu. Chen Zhongrui na Wang Jie kila mmoja amepokea medali ya daraja la tatu ya mafanikio ya anga ya juu, pamoja na cheo cha heshima cha "Mwanaanga Shujaa."

Uamuzi wa kutoa tuzo hizo ulifanywa kwa pamoja na Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Baraza la Serikali la China na Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC).

Chen Dong ameshiriki katika misheni tatu za anga ya juu -- Shenzhou-11, Shenzhou-14 na Shenzhou-20 -- na kukamilisha jumla ya shughuli sita za nje ya chombo (EVAs), na hivyo kuwa mwanaanga wa kwanza wa China kubaki kwenye obiti kwa zaidi ya siku 400.

Chen Zhongrui amefanya shughuli tatu za nje ya chombo wakati wa misheni ya Shenzhou-20, ambayo ilikuwa ni misheni yake ya kwanza ya safari ya anga ya juu.

Mhandisi wa anga ya juu Wang Jie alitimiza majukumu yote aliyopangiwa kwa kiwango cha juu.

Watatu hao walitekeleza shughuli nne za nje ya chombo, kufanya shughuli saba za kuhamisha mizigo kupitia moduli ya kufungia mizigo angani, kukamilisha zaidi ya kazi 120 zinazohusiana na ujenzi, uboreshaji, matengenezo na ukarabati wa kituo cha anga ya juu, pamoja na kufanya mfululizo wa majaribio ya sayansi ya anga ya juu na kuzifanyia teknolojia majaribio.

Chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-20 kilirushwa Aprili 24, 2025, na baadaye kikaunganishwa na kituo cha anga ya juu cha China kwa mafanikio. Kurudi kwake kuliahirishwa mapema Novemba 2025 kutokana na tukio linaloshukiwa kuwa la kugongwa na vifusi vya anga ya juu.

Kufuatia mfululizo wa maandalizi, wanaanga hao wa Shenzhou-20 walirudi salama kwenye dunia tarehe 14 Novemba, 2025, kwa kutumia chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-21.

Siku 11 baadaye, China ilifanya urushaji wa dharura wa chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-22 kisicho na wanaanga, ambacho kinatarajiwa kutumika kama chombo cha kurejea duniani kwa wanaanga watatu wa misheni ya Shenzhou-21 walio obitini kwa sasa.

Wanaanga hao wa misheni ya Shenzhou-20 walikaa siku 204 kwenye obiti, na kuweka rekodi ya muda mrefu zaidi wa kukaa obitini kwa kundi la wanaanga wa China.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha