Lugha Nyingine
Barabara iliyojengwa na kampuni ya China yabadilisha maisha ya watu na kuchochea uchumi kaskazini mwa Rwanda

Picha hii iliyopigwa Januari 21, 2026 ikionyesha gari likisafiri kwenye barabara iliyojengwa na Kampuni ya Barabara na Madaraja ya China (CRBC) katika Mkoa wa Kaskazini wa Rwanda. (Xinhua/Ju Yinhe)
KIGALI - Kwa miaka mingi, vilima vya kaskazini mwa Rwanda vilikuwa vinajulikana si tu kwa uzuri wake wa kuvutia, bali pia kwa safari ndefu na ngumu zilizolazimika kufanywa kupitia barabara zisizopitika. Leo, lami laini ya barabara ya Base-Butaro-Kidaho (BBK) inabadilisha hali hiyo, ikileta matumaini mapya, fursa za kiuchumi, na mabadiliko ya kijamii kwa jamii katika Wilaya ya Burera.
Barabara hiyo ya BBK yenye urefu wa kilomita 63, iliyojengwa kwa pamoja na Kampuni ya Barabara na Madaraja ya China (CRBC) na Kampuni ya NPD ya Rwanda, imekuwa njia ya maisha kwa wakazi, ikipunguza muda wa safari na kufungua uwezo wa maendeleo wa eneo hilo.
"Mradi huu umetusaidia. Naweza kusema ni faida kwetu," amesema Seth Havugimana, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 30 na mkazi wa Kijiji cha Gitare katika Wilaya ya Burera, katika mahojiano ya hivi karibuni na Shirika la Habari la China, Xinhua.
Kabla ya ujenzi wa barabara hiyo, kufikia miji ya karibu ilikuwa changamoto ya kila siku. "Wakati mwingine hatukuweza kufika kabisa kwa sababu ya barabara mbovu," amekumbuka. Safari ambayo hapo awali ilichukua saa nne kufika jiji la Musanze sasa inachukua takribani saa moja.
"Mabadiliko haya yana maana kubwa sana. Biashara sasa inaweza kusonga mbele, na watu wanaweza kusafari kwa urahisi kutoka hapa kwenda mahali pengine. Tunafurahi sana kuhusu barabara hii mpya" amesema.
Kwa Havugimana na wakazi wengine wengi, barabara hiyo ya BBK imebadilisha maisha. Hapo awali alikuwa akifanya safari moja tu kwa siku kwenda Musanze kununua bidhaa, lakini sasa anaweza kufanya zaidi ya safari nne, hivyo kupunguza gharama na kuongeza mapato yake.
"Hapo awali, ilikuwa vigumu kusafiri na kuleta bidhaa au nyenzo hapa. Sasa, mtu akiniambia anahitaji kitu, ninaweza kwenda kukinunua na kukirejesha moja kwa moja" amesema.
Barabara hiyo pia imeboresha upatikanaji wa huduma muhimu. Huku familia zikiwa na uwezo wa kufika shuleni, hospitalini, na masokoni kwa urahisi.
"Ikiwa mtu katika familia yangu ni mgonjwa, ni rahisi kumpeleka hospitalini. Wanafunzi wanaweza kwenda shuleni kwa urahisi. Jambo ambalo hapo awali halikuwezekana" Havugimana amesema.
Jing Niu, kaimu meneja wa mradi wa BBK katika CRBC, amesema kwamba kampuni hiyo ilisimamia ujenzi wa sehemu ya Kidaho-Butaro yenye urefu wa kilomita 22. Amesema, ujenzi huo ulikabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo eneo lenye mwinuko na miamba, ulinzi wa mazingira karibu na Ziwa Burera, usimamizi wa trafiki, na usalama wa watoto.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, kampuni ilifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa na jamii, ikitoa elimu ya usalama mara kwa mara na kuhakikisha barabara inaendelea kutumika ipasavyo.
Mchango wa barabara hiyo ya BBK haukuishia katika maisha ya mtu mmoja mmoja, bali pia umeenea kwenye uchumi mpana wa maeneo ya vijijini.
Thierry Muneza Kamuhanda, mkurugenzi wa mradi wa BBK, amesisitiza kwamba upangaji makini wa mradi huo ulilenga kuleta manufaa ya kijamii na kiuchumi. "Tunakadiria kuwa takriban magari milioni tano hupita hapa kwa mwaka. Pale panapokuwa na trafiki, panakuwa na shughuli za kiuchumi," amesema.
Amesema kuwa mradi huo pia umetoa ajira, huku takriban asilimia 10 ya jumla ya uwekezaji ikitengwa kwa ajili ya wafanyakazi, jambo lililoboresha moja kwa moja mapato ya kaya na hali ya kijamii ya wenyeji.

Mhandisi Mchina Zhou Chunyi (kulia) akifanya kazi na wafanyakazi wenzake wenyeji kando ya barabara iliyojengwa na Kampuni ya Barabara na Madaraja ya China katika Wilaya ya Burera, Mkoa wa Kaskazini wa Rwanda, Januari 21, 2026. (Xinhua/Ju Yinhe)

Wafanyakazi wenyeji wakifanya kazi kando ya barabara iliyojengwa na Kampuni ya Barabara na Madaraja ya China katika Wilaya ya Burera, Mkoa wa Kaskazini wa Rwanda, Januari 21, 2026. (Xinhua/Ju Yinhe)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



