Afrika Kusini yafikiria kutumia jeshi kupambana na magenge ya uhalifu

(CRI Online) Januari 26, 2026

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema serikali inafikiria kutuma jeshi kwenye maeneo yenye vurugu za magenge ya uhalifu ili kukabiliana na uhalifu unaofanywa na magenge hayo.

Rais Ramaphosa amesema hayo siku ya Jumamosi wakati kukiwa na kuongezeka kwa idadi ya vifo vinavyotokana na matukio yanayohusiana na vitendo vya magenge hayo katika sehemu mbalimbali za nchi.

Hata hivyo Rais Ramaphosa ameonya kuwa wanajeshi wamefundishwa kuondoa matishio na si kufanya uchunguzi, kwa hiyo uamuzi wowote wa kutuma wanajeshi unatakiwa kufanywa kwa umakini.

Wikiendi iliyopita watu 26 waliuawa baada ya vurugu za magenge zilizotokea katika Jimbo la Western Cape, pamoja na matukio ya ufyatuaji risasi yaliyosababisha vifo vya watu wengi katika eneo hilo.

Eneo hilo limekuwa na rekodi mbaya ya vurugu za magenge, na takwimu za polisi zinaonyesha kuwa watu 2,104 waliuawa katika eneo la Cape Flats katika miezi tisa ya mwanzo ya 2025.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha