Idadi ya vifo kutokana na matukio yaliyosababishwa na mvua nchini Zimbabwe yaongezeka hadi 109

(CRI Online) Januari 27, 2026

Idara ya Ulinzi wa Wananchi ya Zimbabwe (DCP) imesema watu wasiopungua 109 wamefariki dunia na wengine 61 kujeruhiwa kutokana na mvua inayoendelea kunyesha nchini humo tangu kuanza kwa msimu wa mvua.

Katika ripoti ya hali halisi ya sasa iliyotolewa jana Jumatatu, idara hiyo imesema vifo hivyo vimesababishwa na watu kuzama na kusombwa na maji ya mito iliyofurika, kupigwa radi na kuporomoka kwa migodi.

Kwa mujibu wa idara hiyo, mbali na vifo, mvua hiyo kubwa nchini humo pia imeleta uharibifu mkubwa kwenye miundombinu muhimu, ikiwemo barabara na madaraja, shule, vituo vya afya, nyumba, mabwawa ya maji na miradi ya umwagiliaji.

Idara hiyo imeeleza kuwa sasa inalemewa na hali ya kukabiliana na maafa mbalimbali yaliyoletwa na mvua hiyo inayoendelea.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha