Lugha Nyingine
Hamas yasema kupatikana kwa mwili wa mwisho wa mateka wa Israeli kutoka Gaza kuonesha nia yake ya kusimamisha mapigano
Wanamgambo wa Hamas wakitafuta mwili wa mwisho wa mateka wa Israeli mashariki mwa makazi ya Zeitoun, kusini-mashariki mwa Jiji la Gaza, Januari 7, 2025. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)
GAZA/JERUSALEM - Hamas imesema jana Jumatatu kwamba kupatikana kwa mwili wa mwisho wa mateka wa Israeli katika Ukanda wa Gaza kunaonyesha juhudi zake zote kwa ajili ya kutekeleza makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Katika taarifa moja, msemaji wa Hamas Hazem Qassem amesema Hamas "itaendelea kutekeleza majukumu yote yaliyowekwa kwenye makubaliano hayo," ikiwa ni pamoja na kusaidia kazi ya kamati ya wataalam wanaopewa wajibu wa kusimamia mambo ya Gaza.
Qassem ametoa wito kwa wapatanishi na Marekani kuilazimisha Israeli "kuacha ukiukaji wake wa makubaliano na kutekeleza wajibu wake."
Taarifa hiyo imetolewa wakati Jeshi la Israeli kutangaza kupatikana kwa mwili huo wa Ran Gvili mwenye umri wa miaka 24, ambaye ni askari wa kikosi cha polisi cha Yasam cha Jeshi la Polisi la Israeli, aliyeuawa Oktoba 7, 2023, na baadaye mwili wake kuhamishiwa Gaza.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari kwamba vikosi vya Jeshi la Israeli vilikuwa njiani kurudi Israeli na mwili huo wa Gvili kwa kufanya mazishi, alisema kupatikana kwa mwili huo ni "mafanikio makubwa" kwa Vikosi vya Ulinzi vya Israeli (IDF).
Upande wa jeshi la Israeli umesema, "Kufuatia kukamilika kwa mchakato wa utambuzi uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Matibabu, wawakilishi wa IDF wameiarifu familia ya mateka huyo aliyefariki, Sajenti wa Daraja la Kwanza Ran Gvili, kwamba mpendwa wao ametambuliwa na atarudishwa kwa mazishi".
"Mpaka sasa, mateka wote wamesharudishwa kutoka Ukanda wa Gaza hadi Nchi ya Israeli," taarifa hiyo imeongeza.
Kutangazwa kwa habari hiyo ni siku moja baada ya Israeli kusema imeanzisha "operesheni kubwa" ya kutafuta mwili wa Gvili kwenye makaburi kaskazini mwa Gaza kutokana na habari ya upelelezi.
Taarifa iliyotolewa na Hamas imeeleza kuwa mateka wote wa Israeli sasa wamesharudishwa, ama wakiwa hai au ni miili ya mateka , hii ni sehemu ya kipindi cha kwanza cha makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa Oktoba 2025 chini ya usuluisho wa Marekani, Qatar na Misri.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



