Lugha Nyingine
Iran yasema itatoa jibu "kamilifu na la kuleta majuto" kwa uchokozi wowote

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei akizungumza kwenye mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Januari 26, 2026. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema Jumatatu kwamba Iran itatoa jibu "kamilifu na la kuleta majuto" kwa uchokozi wowote.
Ameyasema hayo kwenye mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, akijibu mienendo ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi pamoja na mazoezi yake ya pamoja yanayoendelea na nchi za Ghuba.
"Tumekuwa, na bado tunaendelea, kukabiliwa na vita mseto. Baada ya uchokozi wa kijeshi wa Israeli dhidi ya Iran mwezi Juni, tumekuwa tukikabiliwa na madai na vitisho vipya kutoka Marekani na Israeli kila siku katika kipindi cha hivi karibuni," Baghaei amesema.
Amesema kwamba nchi za Asia Magharibi zinajua kwamba Iran haitakuwa nchi pekee itakayolengwa na ukosefu wa usalama wa kikanda. "Ukosefu wa usalama unaambukiza," amesema, akiongeza kuwa "nchi yoyote inayoheshimu amani na sheria za kimataifa inapaswa kuchukua msimamo dhahiri juu ya vitisho vya Marekani dhidi ya nchi nyingine."
"Kwa kuzingatia uzoefu wake wa awali wakati wa vita vya siku 12 na Israeli na Marekani, Iran hakika itatoa jibu kamilifu na la kuleta majuto kwa uchokozi wowote," Baghaei ameongeza.
Akitoa maoni juu ya kauli za Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Alhamisi kwamba "kikosi cha majini" cha Marekani kinaelekea Asia Magharibi vikiilenga Iran, Baghaei amesema kuwasili kwa manowari katika eneo hilo "hakupaswi kuathiri azma na umakini wa Iran wa kuilinda nchi."
Ameongeza kuwa vikosi vya Jeshi la Iran vinafuatilia kwa ukaribu maendeleo yoyote na kuboresha kila mara uwezo wao wa kulinda mamlaka ya nchi, hadhi na usalama wa nchi hiyo.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani ili kuzuia vita, Baghaei amesema mazungumzo yanawezekana tu kwa upande ambao hautafuti vita au makabiliano.
"Hatujawahi kukaribisha vita na hatujawahi kuepuka diplomasia na mazungumzo. Tumewahi kuonyesha kwa vitendo," amesema.
Kuongezeka kwa uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo kunafuatia Trump kuunga mkono hivi karibuni maandamano ya kupinga serikali nchini Iran, ambapo alisema, "Usaidizi unakuja."
Alhamisi wiki iliyopita, Trump alitangaza kwamba kikosi "kikubwa" cha majini cha Marekani kinaelekea Iran, huku akidai kwamba huenda kisitumike.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei akihudhuria mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Januari 26, 2026. (Xinhua/Shadati)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



