Lugha Nyingine
China yaahidi kuwa "soko la dunia" huku ikiendeleza ufunguaji mlango wa kiwango cha juu

Watalii wa kigeni wakitembelea soko mjini Sanya, Mkoani Hainan, kusini mwa China, Januari 11, 2026. (Xinhua/Guo Cheng)
BEIJING - China, zaidi ya kuitwa "kiwanda cha dunia." ina nia ya kuwa "soko la dunia," huku soko lake kubwa sana likitoa fursa pana kwa bidhaa na huduma kutoka nchi zote, Wizara ya Biashara ya China imesema, ikieleza mipango yake ya kuimarisha uhusiano wa uwekezaji na biashara katika mwaka 2026.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing jana Jumatatu, wizara hiyo imesema kwamba China itaendelea kusukuma mbele ufunguaji mlango wa kiwango cha juu mwaka huu, na itaendelea kuingiza msukumo mpya katika uchumi duniani kupitia maendeleo yake yenye sifa bora.
Katika kusukuma mbele ufunguaji mlango wa kiwango cha juu, wizara hiyo ya biashara imedhamiria kuboresha zaidi sera za kunga mkono uwekezaji wa kigeni katika mwaka 2026, ikiahidi juhudi za kutoa huduma sawa kwa kampuni zilizowekezwa na mtaji wa kigeni katika mipango ya kuhimiza matumizi ya ndani, manunuzi ya serikali, na michakato ya zabuni za umma ili kuhimiza maendeleo ya muda mrefu ya kampuni za kigeni nchini humo.
Wang Ya, afisa anayeongoza idara ya usimamizi wa uwekezaji wa kigeni chini ya wizara ya biashara, amesema kwenye mkutano huo na waandishi wa habari kwamba China itaendelea bila kuyumba kupanua ufunguaji mlango wa kiwango cha juu inapotafuta kukuza nguvu mpya katika kuvutia uwekezaji wa kigeni na kuboresha chapa ya "Wekeza nchini China".
Wang amesema wizara hiyo itapanua ufikiaji wa soko na ufunguaji mlango wa sekta ya huduma, zikiwemo za mawasiliano ya simu, huduma ya afya na elimu. Pia itaunga mkono kampuni zinazowekezwa na mtaji wa kigeni kwenye sekta ya huduma katika kupanua minyororo yao ya thamani.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, China itaendelea kuhimiza ushirikiano wa biashara huria na Baraza la Ushirikiano la Ghuba, Uswisi, Korea Kusini, New Zealand, nchi za Visiwa vya Pasifiki, na nchi za Asia ya Kati na Afrika katika mwaka 2026. Pia itaharakisha mazungumzo kuhusu mikataba ya uwekezaji, hasa makubaliano na nchi washirika wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI).
Kwenye mkutano huo huo na waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Biashara wa China Yan Dong amesema kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kuboresha ushirikiano wa uwekezaji wa pande mbili, akisema kuwa China inatafuta kupanua ushirikiano wake katika sekta zinazoibukia kama vile madini ya kijani, nishati safi, uchumi wa kidijitali na AI na nchi washirika wa BRI.
"China itaendelea kusukuma mbele miradi kinara vilevile mipango ya maisha ya watu ya 'midogo lakini yenye ubora' ili kusaidia nchi washirika wa BRI kuboresha miundombinu yao, uzalishaji na hali ya maisha," Yan amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



