Lugha Nyingine
Rais Xi akaribisha kampuni za Finland "kuogelea katika bahari kubwa ya soko la China"

Rais wa China Xi Jinping akikutana na Waziri Mkuu wa Finland Petteri Orpo, ambaye yuko katika ziara rasmi nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, Januari 27, 2026. (Xinhua/Li Xiang)
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping jana Jumanne kwenye mkutano wake mjini Beijing na Waziri Mkuu wa Finland Petteri Orpo amekaribisha kampuni za Finland "kuogelea katika bahari kubwa ya soko la China" ili kuongeza nguvu ya kufanya ushindani duniani, akitoa wito kwa pande zote mbili kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana kwenye maeneo ya kubadilisha muundo wa nishati, uchumi wa mzunguko, sekta za kilimo na misitu, na uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia.
Rais Xi amesema kwamba Finland ilikuwa moja kati ya nchi za kwanza kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Jamhuri ya Watu wa China, na katika miaka 76 iliyopita tangu kuanzishwa kwa uhusiano huo wa kidiplomasia, uhusiano kati ya China na Finland ulikuwa wa kuheshimiana, kuwa na usawa, kutupia macho siku za baadaye, na kufanya ushirikiano wa kunufaishana ili kutafuta maendeleo kwa pamoja, na umepata ukuaji tulivu bila kujali hali ya kimataifa inavyobadilika kwa namna gani.
Xi amesema, mwaka huu ni mwanzo wa kipindi cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China, China itaendelea kusukuma mbele maendeleo yenye sifa bora na kupanua ufunguaji mlango wa kufuata vigezo vya juu.
Xi amesema, "Finland ni nchi yenye nguvu kubwa katika michezo ya majira ya baridi, na China pia imeibuka kuwa nchi kubwa ya michezo ya majira ya baridi," akitoa wito kwa pande zote mbili kuhimiza mawasiliano na ushirikiano katika michezo hiyo na kuendeleza urafiki wao katika michezo ya majira ya baridi.
Amekaribisha watu wengi zaidi wa Finland kutembelea China na kujionea hali ya mafungamano ya urithi wa utamaduni wa kale na nguvu hai za mambo ya kisasa nchini China.
Wakati huo huo, Rais Xi amesema, katika dunia inayokabiliwa na hatari na changamoto mbalimbali, jumuiya ya kimataifa inapaswa kuungana mkono kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo, akiongeza kuwa nchi kubwa zinapaswa kuwa mfano mzuri wa kuhimiza usawa, kufuata utawala wa kisheria, kutafuta ushirikiano, na kushikilia uadilifu.
Amesema, China inapenda kushirikiana na Finland katika kushikilia kithabiti mfumo wa kimataifa ambao Umoja wa Mataifa ni kiini chake, na utaratibu wa kimataifa uliowekwa kwenye msingi wa sheria za kimataifa, ili kukabiliana kwa pamoja na changamoto za kimataifa.
Orpo amesema kuwa kampuni za Finland zina shauku kubwa ya kuja China kwa ushirikiano, na Finland ina nia ya kushirikiana na China kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na marais wawili wa nchi hizo mbili, kuongeza mawasiliano ya ngazi ya juu, na kuzidisha ushirikiano wa kufuata hali halisi katika biashara, uwekezaji, uchumi wa kidijitali, nishati safi, na kilimo.
Orpo pia amesema, Finland inafuata sera ya kuwepo kwa China moja. Ameongeza kuwa Finland inasifu kazi muhimu ya kiujenzi iliyofanywa na China katika mambo ya kimataifa, na ina nia ya kuimarisha mawasiliano na uratibu na China, na kulinda kwa pamoja amani na utulivu duniani.

Rais wa China Xi Jinping akikutana na Waziri Mkuu wa Finland Petteri Orpo, ambaye yuko katika ziara rasmi nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, Januari 27, 2026. (Xinhua/Liu Bin)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



