Lugha Nyingine
Botswana yatenga mfuko wa mwitikio wa dharura kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa FMD kwa kuvuka mipaka
Botswana imeidhinisha mfuko wa mwitikio wa dharura wa takriban Dola milioni 7 za Marekani ili kuzuia mlipuko wa homa ya midomo na kwato kwa wanyama (FMD) baada ya kupata taarifa kutoka nchi jirani kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo.
Kwenye hotuba kwa taifa iliyorushwa moja kwa moja kupitia televisheni jana Jumanne mjini Gaborone, Waziri wa Mawasiliano na Uvumbuzi wa Botswana Bw. David Tshere amesema kuwa tahadhari rasmi kutoka serikali za Afrika Kusini na Zimbabwe, ambako mlipuko wa ugonjwa huo unaendelea, imesababisha kuchukuliwa kwa hatua hizo za dharura.
"Ugonjwa huo umeshabainika umbali wa kilomita takriban 10 kutoka kwenye mipaka yetu na nchi zote mbili za Afrika Kusini na Zimbabwe. Ukaribu huu unaleta tishio kubwa na la haraka kwa mifugo yetu na uchumi wa kilimo wa taifa" amesema.
Ameongeza kuwa tayari mamlaka za Botswana zimeua na kuchoma ng'ombe takriban 48 waliovuka mpaka kwenda katika nchi hizo zilizo na maambukizi tangu mwezi huu uanze.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



