Lugha Nyingine
Pilika za usafiri wakati wa Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China zaanza na idadi ya wasafiri yakadiriwa kuvunja rekodi (2)
![]() |
| Picha iliyopigwa Februari 1, 2026 ikionyesha treni za mwendo-kasi kwenye kituo cha treni katika Mji wa Wuhan, Mkoa wa Hubei, katikati mwa China. (Xinhua/Wu Zhizun) |
BEIJING – Majira ya saa 6:40 usiku jana Jumatatu, treni No. K4069 iliondoka kutoka Stesheni ya Reli ya Magharibi ya Beijing, na kuwa treni ya kwanza ya abiria kuondoka Beijing katika pilika za usafiri za Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China 2026. Ndani ya treni hiyo walikuwemo wasafiri wanaorudi nyumbani au wanaofunga safari za kwenda mapumzikoni, na wakati huu ndipo simulizi ya mwaka kuhusu usafiri wa watu na kujumuika pamoja na familia nchini China inapoanza rasmi.
Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China itakuwa Tarehe 17 Februari mwaka huu, na serikali imeamua mapumziko ya siku tisa ya sikukuu hiyo kwa watu wote wanaofanya kazi. Pilika za safari za abiria katika kipindi cha sikukuu hiyo zinaitwa "Chunyun", na katika lugha ya Kichina maana yake ni "pilika za ushafirishaji wa Spring". Pilika hizo huelezwa kuwa ni usafiri wa watu wengi zaidi duniani, na katika pilika hizo za mwaka huu, safari za abiria kati ya maeneo tofauti nchini humu zinakadiriwa kuvunja rekodi ya bilioni 9.5 katika siku 40 kuanzia jana Jumatatu hadi Machi 13.
Kati ya idadi ya jumla ya wasafiri hao, idadi ya wasafiri wanaoendesha magari yao barabarani itaendelea kuchukua nafasi ya kwanza na kufikia asilimia takriban 80.
Idara husika zimekadiria kuwa, reli za kote nchini zitasafirisha abiria milioni 540, na usafiri wa ndege za abiria utafikia mara milioni 95. Ukubwa wa jumla wa usafirishaji wa abiria kwenye njia za reli na anga wakati wa kilele cha trafiki cha siku unakadiriwa kufikia rekodi mpya ya juu katika historia.
Ingawa idadi ya abiria inakadiriwa kufikia kilele kipya, usafiri wao utakuwa mzuri na kuratibiwa vema zaidi.
Mamlaka ya serikali imesema kuwa, barabara za mwendo kasi nchini China sasa zinafika katika asilimia 99 ya sehemu zote zenye idadi ya watu zaidi ya 200,000, na urefu wa mtandao wa reli za mwendo-kasi nchini China umezidi kilomita 50,000, ukifika katika asilimia 97 ya miji yenye idadi ya watu mijini zaidi ya 500,000. Huduma za usafiri wa anga, kwa sasa, zinafika katika asilimia 92.6 ya maeneo ya ngazi ya kiwilaya ya China.
Wakati wa pilika za mwaka huu za usafiri, mamlaka za usafiri zitatumia zaidi nguvu bora za mfumo wa jumla wa usafiri na kuboresha huduma za jumla za mawasiliano barabarani, njia za reli na angani.
"Idara za reli, barabara, njia za maji na usafiri wa ndege za abiria zitaimarisha uchambuzi wa mahitaji ya abiria na kuongeza uwezo wa kusafirisha abiria katika maeneo muhimu, kwenye njia zinazotumiwa na watu wengi zaidi na wakati wa saa za wasafiri wengi, ili kukidhi mahitaji ya watu ya usafiri," amesema Li Chunlin, naibu mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




