Lugha Nyingine
Visa vya Ebola nchini DRC vyafikia 363, huku Uganda ikiripoti watu wanne waliopona (4)
![]() |
| Wafanyakazi wa matibabu wakiandaa chakula kwa watu walio chini ya karantini mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 4, 2026. (Xinhua) |
KINSHASA - Visa vilivyothibitishwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) vimeongezeka hadi 363, ikiwa ni pamoja na vifo 62, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Jumatano na serikali ya DRC, huku Uganda jana Alhamisi ikiripoti watu wanne waliopona.
Hali hiyo mpya imejadiliwa jana Alhamisi kwenye mkutano na waandishi wa habari mtandaoni ulioandaliwa na Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, ambao uliwakutanisha maafisa waandamizi wa WHO na wawakilishi wa serikali kutoka DRC, Uganda na Sudan Kusini.
Mlipuko huo, uliosababishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo, ulitangazwa nchini DRC na Uganda Mei 15. Baadaye WHO iliutangaza kuwa dharura ya afya ya umma inayohitaji umakini na ufuatiliaji kimataifa.
"Hapo awali virusi hivyo vilituacha kwa kasi. Lakini tunavikaribia. Tayari tunaona upigaji hatua," Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Mohamed Janabi ameuambia mkutano huo.
Janabi amesema wagonjwa sita wametibiwa kwa mafanikio na kuruhusiwa kutoka hospitalini nchini DRC, huku watu waliopona pia wakirekodiwa nchini Uganda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Uganda Diana Atwine amesema nchi hiyo hadi sasa imethibitisha visa 15 vya Ebola, ikiwemo visa 11 vilivyoingizwa nchini na maambukizi manne miongoni mwa wafanyakazi wa afya waliomtibu mgonjwa wa kwanza. "Kati yao, pia tumeruhusu wanne kutoka hospitalini."
Amesema Uganda imefuatilia watu 620 waliokutana na watu wanaoshukiwa kuambukizwa, ambapo 270 wamekamilisha kipindi cha uchunguzi wa siku 21 kinachohitajika na wameruhusiwa kutoka kwenye ufuatiliaji, huku wengine bado wakifuatiliwa.
Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba amesema uwezo uliopanuliwa wa uchunguzi unasaidia mamlaka kutoa takwimu sahihi zaidi na kukabiliana kwa haraka zaidi katika maeneo yaliyoathiriwa.
"Jambo muhimu kwa sasa ni kuwa na upimaji mzuri," amesema, akibainisha kuwa upimaji umeanza karibu zaidi na maeneo yaliyoathirika zaidi, na kuruhusu visa vinavyoshukiwa kuthibitishwa kwa haraka zaidi.
Maafisa wa WHO wamesema DRC inagatua hatua za kukabiliana na ugonjwa kwenye ngazi ya maeneo ya kiafya, huku mifumo ya uratibu wa papo hapo, timu za kukabiliana kwa haraka na mifumo ya tahadhari ikiimarishwa katika maeneo yaliyoathiriwa.
Janabi, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, amesema mlipuko huo umeonyesha tena kwamba ushirikiano wa kikanda ni muhimu, akibainisha kuwa kisa cha kwanza kilichotambuliwa nchini Uganda kilitoka DRC baada ya mgonjwa kuvuka mpaka kutafuta huduma katika kituo cha afya kilicho karibu.
Amekosoa vizuizi vikubwa vya usafiri na kufungwa kwa mipaka vilivyowekwa ili kukabiliana na mlipuko huo.
Amezihimiza nchi kuimarisha upimaji kwenye maeneo rasmi ya kuvukia mipaka badala ya kusukuma wasafiri kuelekea njia zisizo rasmi ambako upimaji wa afya ni mgumu zaidi.

Meli kubwa ya kitalii ya pili kuundwa ndani ya China yakamilisha jaribio la kwanza la baharini

Hifadhi ya Taifa ya Kruger ya Afrika Kusini yaadhimisha miaka 100

Nishati ya kijani yahimiza maendeleo yenye sifa bora katika Mkoa wa Xizang, China

Madaraja ya matao yenye mapaa ya mbao yahifadhiwa vizuri katika Mkoa wa Fujian, China
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma
