Lugha Nyingine
Rais wa China afanya mazungumzo na Rais wa Myanmar juu ya kuimarisha ushirikiano
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo na Rais wa Myanmar Min Aung Hlaing mjini Beijing jana Jumanne akisema kwamba China inaweka uhusiano na Myanmar kama kipaumbele katika diplomasia ya ujirani, na inaiunga mkono serikali mpya ya Myanmar katika kuratibu mahitaji ya maendeleo na usalama, na kutafuta njia sahihi ya maendeleo inayolingana na hali halisi ya nchi yake na inayoungwa mkono na umma.
Xi amesema kwamba China inashikilia kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, inafuata sera ya urafiki kwa watu wote wa Myanmar, na inaiunga mkono kithabiti Myanmar katika kulinda mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi yake.
Xi akieleza kuwa mwaka huu ni mwanzo wa utekelezaji wa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China (2026-2030), China inapenda kunufaika pamoja na Myanmar na uzoefu wake wa maendeleo, na kujenga kwa pamoja jumuiya ya China na Myanmar yenye mustakabali wa pamoja kwenye msingi wa hali ya kirafiki na kuaminiana kisiasa, maendeleo ya kunufaishana, uratibu wa usalama na mawasiliano kati ya watu na watu.
"China inaunga mkono pande zote nchini Myanmar katika kusukuma mbele amani na maafikiano kwa kupitia mazungumzo ili kufikia utulivu wa kudumu kaskazini mwa Myanmar, haya yote yanalingana na maslahi ya kimsingi na ya muda mrefu ya Myanmar na watu wake", amesema.
Min Aung Hlaing amepongeza uhusiano wa kirafiki wa "pauk-phaw" unaoendelea kwa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili, na kuishukuru China kwa uungaji wake mkono wa muda mrefu na usio na ubinafsi kwa maendeleo, utulivu, amani na maafikiano ya Myanmar, akiongeza kuwa Myanmar itafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja.
Min Aung Hlaing amesema kuwa utekelezaji wa China wa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano unaleta fursa muhimu kwa majirani zake wa Asia ikiwemo Myanmar, na Myanmar inatumai kuzidisha ushirikiano wa pande zote na China, kujenga kwa pamoja Ushoroba wa Kiuchumi wa Myanmar-China na kuinua kiwango cha ushirikiano wa biashara na uwekezaji wa pande mbili.
"Myanmar inaunga mkono kikamilifu mapendekezo manne makubwa ya dunia yaliyotolewa na Rais Xi, na iko tayari kuzidisha mawasiliano na uratibu wa pande nyingi na China," amesema.
Baada ya mazungumzo hayo, marais hao wawili walishuhudia kwa pamoja kusainiwa kwa nyaraka za ushirikiano katika mawasiliano na uchukuzi, na katika mambo ya maisha ya watu.
Kabla ya mazungumzo, Xi alifanya hafla ya kumkaribisha Min Aung Hlaing. Dhifa ya kumkaribisha pia ilifanyika majira ya mchana.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




