Lugha Nyingine
Shanghai Disneyland yasherehekea maadhimisho ya miaka 10 huku vivutio vipya vikiwa mbioni kuja (2)
SHANGHAI - Huku Shanghai Disneyland, bustani ya burudani na starehe mjini Shanghai, mashariki mwa China ikiadhimisha miaka 10 tangu kuzinduliwa kwake jana Jumanne, eneo hilo la mapumziko linasonga mbele na mipango kadhaa ya upanuzi, baada ya kukaribisha watembeleaji zaidi ya milioni 100 hadi ilipofika mwisho wa Oktoba 2025.
Juzi Jumatatu, Andrew Bolstein, rais na meneja mkuu wa Eneo la Mapumziko la Disney la Shanghai (Shanghai Disney Resort), alitoa taarifa zaidi juu ya ardhi mpya ya Shanghai Disneyland yenye mandhari ya mambo ya Spider-Man, ambayo itakuwa ardhi ya tisa ya mandhari ya bustani hiyo. Sehemu ya mwisho ya njia ya nyekundu ambayo ni alama ya kivutio hicho iliwekwa hivi karibuni.
Aidha, amesema hoteli ya tatu ya eneo hilo la mapumziko, Hoteli ya Shanghai Disney Enchanted Star, imepangwa kufunguliwa majira ya baridi ya mwaka huu.
Bustani hiyo imefaidika na ongezeko la kasi la utalii wa Shanghai. Pia imetoa ajira zaidi ya 15,000 za moja kwa moja katika mji huo.
Mwaka 2011, wakati ujenzi wa Eneo la Mapumziko la Disney la Shanghai ulipoanza kwa mara ya kwanza, Shanghai ilipokea watalii milioni 230 wa ndani na kupata mapato ya utalii ya yuan takriban bilioni 278.6 (dola za Marekani karibu bilioni 40.92). Kufikia mwaka 2025, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi watalii milioni 416 wa ndani na mapato ya yuan bilioni 566.68, kwa mujibu wa mamlaka za utamaduni na utalii za mji huo.
Utalii unaoongezeka wa watalii wa kigeni wanaoingia China, ukichochewa na sera zinazopanuka za kuingia bila visa, pia umeongeza mahudhurio katika Shanghai Disneyland, hasa miongoni mwa watalii kutoka Japan, Jamhuri ya Korea, na nchi za Asia Kusini-Mashariki.
Mtalii wa Thailand Aum, ambaye ameshatembelea Shanghai Disneyland mara mbili, amesema amevutiwa na hali ya hewa nzuri ya Shanghai, gharama nafuu na usafiri wake rahisi. Amesema bustani hiyo inatoa safari za kufurahisha, burudani mbalimbali na machaguo ya aina mbalimbali za chakula.
Tangu majira ya mchipuko ya mwaka huu, Eneo la Mapumziko la Disney la Shanghai limefanya mfululizo wa shughuli kusherehekea maadhimisho yake hayo ya miaka 10. Wakati likizo ya majira ya joto ikikaribia, bustani za burudani na starehe kote Shanghai, ikiwemo eneo hilo la mapumziko, zinatarajiwa kushuhudia ongezeko la watembeleaji.
"Tuliamini tunaweza kutengeneza kitu fulani ambacho dunia haijawahi kukiona -- mahali ambapo usimuliaji wa Disney unakutana na utamaduni wa Kichina kwa njia ambayo ilikuwa kiuhalisia mpya," amesema Josh D'Amaro, afisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Walt Disney. "Tunaposherehekea muongo wa kwanza wa bustani hii na kutazamia hatua inayofuata, kinachonifurahisha zaidi ni kwamba ndiyo tu tunaanza."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




