Wang Yi atoa wito wa kurejeshwa mapema kwa hali ya kawaida ya usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 25, 2026

BEIJING – Usafirishaji wa kawaida kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz unapaswa kurejeshwa mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha utulivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji duniani, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema katika mazungumzo kwa njia ya simu jana Jumatano na Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Ishaq Dar.

Kwenye mazungumzo hayo, Wang ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ameushukuru upande wa Pakistan kwa kuiarifu China haraka kuhusu hatua mpya ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani. Amesema kwamba kusainiwa kwa nyaraka ya makubaliano (MoU) kati ya nchi hizo mbili ni matokeo ya juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa, na Pakistan imebeba jukumu muhimu na la kipekee ndani yake.

"Mchakato wa amani ndiyo tu umeanza, na bado kuna safari ndefu, hata ya mahangaiko na ngumu mbele," Wang amebainisha, akisisitiza kwamba China, kama kawaida, itaiunga mkono Pakistan na nchi zingine zenye nia moja katika kuendelea kubeba jukumu la kiujenzi, na iko tayari kudumisha mawasiliano na uratibu wa karibu na Pakistan.

Wang ametaja vipaumbele vitatu muhimu katika hatua inayofuata.

Amesema kwanza, ni muhimu kuimarisha usimamishaji mapigano kamili na kukomesha vita, na chini ya hali yoyote ile vita visijirudie tena.

"MoU ya Iran na Marekani inaendana na maslahi ya msingi na ya muda mrefu ya Iran, vilevile matarajio ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa," Wang amesema, akiongeza kuwa China ina nia ya kufanya kazi na pande zote ili kuunga mkono kithabiti mazungumzo yasonge mbele bila uingiliaji.

Pili, Wang amesema usafirishaji wa kawaida kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz unapaswa kurejeshwa haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha kuna utulivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji duniani. Ameongeza kuwa mipangilio kuhusu mlango-bahari huo inapaswa kuheshimu mamlaka ya nchi na haki na maslahi halali ya mataifa yanayopakana na mlango-bahari huo, ikifuata desturi za kimataifa na matarajio ya pamoja ya nchi zote.

Tatu, Wang amesema juhudi zinapaswa kufanywa ili kusaidia nchi za Mashariki ya Kati katika kuboresha uhusiano wao na kuchunguza muundo mpya wa usalama wa kikanda.

Ameeleza kuwa Mashariki ya Kati, likiwemo eneo la Ghuba, hazipaswi tena kutumika kama uwanja wa ushindani wa mataifa yenye nguvu kubwa au mwathirika wa siasa za kijiografia, na nchi za kikanda zinapaswa kudumisha kujitegemea hasa kimkakati na bila kuyumbayumba kuweka mustakabali wao mikononi mwao wenyewe. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha