Lugha Nyingine
Wito wa amani na mshikamano wa kijamii wasikika katika vitongoji vya Afrika Kusini kabla ya maandamano ya kupinga uhamiaji

Picha iliyopigwa Juni 12, 2026 ikionyesha mandhari ya Soweto kusini-magharibi mwa Johannesburg, Afrika Kusini. (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)
JOHANNESBURG - Zikiwa zimebakia siku chache kabla ya maandamano ya kupinga uhamiaji yaliyopangwa kufanyika kote Afrika Kusini Juni 30, wakazi wengi katika vitongoji vya Johannesburg wanasema hawana nia ya kushiriki, wakisisitiza badala yake umuhimu wa amani, mshikamano wa kijamii, na utulivu wa kiuchumi.
Maandamano hayo, yanayoandaliwa na kundi linalojulikana kwa jina la March and March, yamekuwa yakitangazwa kuwa sehemu ya kukabiliana na masuala kuhusu uhamiaji haramu, uhalifu, na ukosefu wa ajira.
Hata hivyo mahojiano yaliyofanywa na Shirika la Habari la China, Xinhua katika vitongoji vikiwemo vya Soweto, Alexandra, Tembisa, na Diepsloot yanaonesha mtazamo tofauti, huku wakazi wengi wakisema kwamba maandamano mara nyingi huvuruga shughuli za kujipatia kipato na biashara ya vitongoji husika huku yakifanya juhudi chache kushughulikia changamoto za msingi.
"Tumewahi kuandamana hapo awali, lakini hali yangu haijabadilika sana. Nina watoto wanaonitegemea. Kwa hivyo kwa sasa, bora nijikite katika kutafuta kazi na kuweka chakula mezani," amesema mkazi wa Soweto Mhlabeni Dube mwenye umri wa miaka 46.
Katika kitongoji cha Alexandra, mchuuzi wa mtaani Nombulelo Hlatshwayo amesema kudumisha amani ni muhimu zaidi kuliko kuingia barabarani kuandamana.
"Tunaweza kuwa tunatoka asili tofauti, lakini tunaishi pamoja kila siku na tunahitaji kutafuta njia za kuelewana," amesema, akiongeza kuwa jamii tayari zimeshakabiliwa na changamoto za kutosha na hazihitaji vurugu au mgawanyiko.
Baadhi ya wakazi pia wameelezea kwamba mchango wa raia wa kigeni katika uchumi wa vitongoji haupaswi kupuuzwa, wakibainisha kuwa biashara nyingi zinazomilikiwa na wahamiaji hutoa bidhaa na huduma muhimu wakati huohuo zinachochea shughuli za kiuchumi katika jamii zisizopata huduma za kutosha.
"Kile jamii zinahitaji hasa ni kazi na suluhisho za kivitendo, si maandamano," amesema mkazi wa Alexandra mwenye umri wa miaka 34 Lindokuhle Gasa.

Picha iliyopigwa Juni 24, 2026 ikionyesha mandhari ya Alexandra, Johannesburg, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)
Katika wiki za hivi karibuni, mivutano inayohusishwa na hisia za kupinga wahamiaji imeibuka katika jamii kadhaa kote nchini humo, huku kukiwa na ripoti za mashambulizi na uporaji unaolenga baadhi ya biashara zinazomilikiwa na wageni.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, raia haramu wa kigeni takriban 40,000 wameshakamatwa tangu mwanzo wa mwaka, wakati huohuo maelfu ya raia kutoka Malawi, Zimbabwe, Msumbiji, Ghana, na Nigeria wamerudishwa makwao.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (kushoto) akihutubia maadhimisho rasmi ya Siku ya Kitaifa ya Vijana, Johannesburg, Afrika Kusini, Juni 16, 2026. (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)
Mamlaka za Afrika Kusini zimekuwa zikilaani mara kwa mara vitendo vya vurugu na kusisitiza kwamba masuala yanayohusiana na uhamiaji yanapaswa kushughulikiwa kupitia njia za kisheria.
Akihutubia maadhimisho rasmi ya Siku ya Kitaifa ya Vijana Juni 16, rais wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa, alisema serikali ilikuwa ikishughulikia changamoto zinazowakabili Waafrika Kusini na kuonya dhidi ya majaribio ya kuchochea hali ya ukosefu wa utulivu.
"Maandamano ya Juni 30, kwa maoni yangu, si tukio ambalo ni muhimu hata kidogo kwa sababu tunashughulikia changamoto ambazo watu wetu wanakabiliana nazo," alisema, akiongeza kwamba "hatupaswi kuruhusu Waafrika Kusini kulaghaiwa na kupotoshwa na wale wanaotaka kujenga hali ya ukosefu wa utulivu katika nchi yetu na hatutaruhusu hilo."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



