Lugha Nyingine
Wazimbabwe wataka kurejeshwa nyumbani haraka mjini Cape Town wakati tarehe ya mwisho ya kupinga wahamiaji ikikaribia

Waafrika Kusini wakiwa wamekusanyika nje ya Bunge kwa maandamano ya kupinga chuki dhidi ya wageni mjini Cape Town, Afrika Kusini, Juni 27, 2026. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)
CAPE TOWN – Wazimbabwe zaidi ya 500 wamekusanyika nje ya ubalozi mdogo wa nchi yao mjini Cape Town wakitaka kurejeshwa nyumbani kwa usaidizi wa serikali, wakati hofu ikizidi kuongezeka juu ya maandamano ya kupinga wahamiaji yaliyopangwa kufanyika kesho Juni 30 ambayo yamesababisha raia wengi wa kigeni kutaka kuondoka Afrika Kusini.
Makundi ya kupinga wahamiaji yameweka tarehe ya mwisho isiyo rasmi ya Juni 30 kwa raia wa kigeni wasio na vibali kuondoka nchini humo kwa hiari, wito ambao mara nyingi umekuwa ukiambatana na vitisho vya vurugu na kushambuliwa kimwili kwa raia wa kigeni, bila kujali hali yao ya uhamiaji.
Familia zilizobeba mabegi yaliyofungwa kwa plastiki zimejaa kwenye ubalozi mdogo huo wa Zimbabwe, mitaa ya jirani na bustani ya karibu huku idadi ya watu ikiendelea kuongezeka. Baadhi walikuwa wamelala kwenye njia za simenti nje ya ubalozi huo kabla ya kuhamia katika jengo la ubalozi kadri nafasi ilivyozidi kupatikana. Mabasi kila baada ya muda yalichukua baadhi ya raia kuwarudisha nyumbani huku watu wengi zaidi wakiendelea kuwasili.
Mashirika ya kibinadamu yalisambaza chakula na misaada mingine katika eneo hilo huku serikali za mitaa, mikoa na kitaifa zikiwa hazikutoa msaada wowote. Watoto, wakiwemo watoto wachanga, walionekana nje kwenye baridi kali wakati ambapo halijoto zilikuwa zikitabiriwa kushuka na mvua kubwa kunyesha jana Jumapili.
Mashirika ya kibinadamu yameonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu, yakirejelea hatari kubwa za kiafya kutokana na mamia ya watu kuendelea kuwa wamejazana pamoja bila usafi wa kutosha, maliwato au miundombinu ya usafi.
Mgcini Sibanda, raia wa Zimbabwe aliye nje ya ubalozi huo, amesema anataka kuondoka Afrika Kusini kwa sababu hana nyaraka na kazi.
"Sina nyaraka, sababu ya kwanini ni kwa sababu si rahisi kupata nyaraka kama uko Zimbabwe kwa sababu ni ghali sana. Ndiyo maana watu wengi hawana nyaraka. Hasa pasipoti, ni ghali sana. Tunapokuja hapa, tena tunahangaika kupata kibali cha kufanya kazi," amesema.
Hali kama hiyo imeonekana nje ya Ubalozi wa Malawi jijini Johannesburg, ambapo mamia ya raia wa Malawi wamekusanyika wakitafuta usaidizi wa kurejea nyumbani kabla ya tarehe hiyo ya mwisho ya Juni 30.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari Ijumaa, Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Ronald Lamola alisema sheria za uhamiaji lazima zitekelezwe na mamlaka za uhamiaji na mashirika mengine husika ya serikali, si na watu au jumuiya binafsi.
"Kinachokuwa tatizo kwetu kimataifa, ni makundi yanayotembea nyumba hadi nyumba yakitekeleza sheria na maandamano ya vurugu wakati mwingine ambayo hulazimisha baadhi ya raia wa kigeni kuonyesha aina yoyote ya nyaraka," Lamola amesema.
Nje ya Bunge mjini Cape Town siku ya Jumamosi, Waafrika Kusini kadhaa walikusanyika kwa maandamano ya kupinga chuki dhidi ya wageni, wakikataa tarehe hiyo ya mwisho isiyo rasmi na mashambulizi yanayolenga raia wa kigeni.
Wakati huo huo, watu takriban 100 katika mji wa pwani wa Hermanus waliandamana dhidi ya raia wa kigeni wasio na nyaraka siku ya Jumamosi, wakitoa wito wa Waafrika Kusini kuajiriwa badala ya raia wa kigeni. Polisi walifyatua mabomu ya kuwatawanya baada ya waandamanaji kukataa amri za polisi za kuweka chini silaha hatari.

Wazimbabwe wakiwa wamekusanyika nje ya Ubalozi mdogo wa Zimbabwe wakitaka kurejeshwa nyumbani kwa usaidizi wa serikali, Cape Town, Afrika Kusini, Juni 27, 2026. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)

Wazimbabwe wakiwa wamekusanyika nje ya Ubalozi mdogo wa Zimbabwe wakitaka kurejeshwa nyumbani kwa usaidizi wa serikali, Cape Town, Afrika Kusini, Juni 27, 2026. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



