Lugha Nyingine
Xi Jinping akutana na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko

Rais wa China Xi Jinping akikutana na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko kwenye Jumba la Kupokea Wageni wa Kitaifa la Diaoyutai, hapa Beijing, mji mkuu wa China, Juni 29, 2026. (Xinhua/Shen Hong)
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amekutana na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko mjini Beijing Jumatatu, akisisitiza kwamba China na Belarus zinapaswa kudumisha mawasiliano ya kimkakati, na kuhimiza uhusiano wa pande mbili unaoendelea kwenye kiwango cha juu uendelezwe hatua kwa hatua ili kuleta manufaa mazuri zaidi kwa watu wa nchi hizo mbili.
"China inaiunga mkono Belarus katika kulinda mamlaka ya nchi, uhuru na ukamilifu wa ardhi, na kufuata njia yake ya kujiendeleza inayolingana na hali halisi ya nchi," Xi amesema, akielezea nia ya China ya kuendelea kutoa msaada kwa iwezekanavyo kwa maendeleo ya Belarus.
Xi amesema China na Belarus ni marafiki wa kweli wanaoaminiana na kuungana mkono, ni washirika wazuri katika kutafuta maendeleo na ustawi kwa pamoja, na ni washirika wa kimkakati wa pande zote na katika hali yoyote.
Amesema baada ya kuhimili majaribu ya mabadiliko ya hali ya kimataifa, uhusiano wa pande mbili umepata maendeleo kwa kupiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni, na sasa umeingia katika kipindi bora zaidi katika historia.
Xi amesema pande hizo mbili zimekuwa zikifurahia kuaminiana imara kisiasa, zimepata matokeo yenye matunda katika ushirikiano wa sifa bora wa ujenzi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, zimepata maendeleo ya kihalisi katika miradi muhimu ya ushirikiano, na zimefanya uratibu wa pande nyingi wenye ufanisi.
"Nchi hizo mbili zinapaswa kuhamasisha rasilimali kutoka sekta mbalimbali ili kusukuma mbele ushirikiano wa ujenzi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, na kuongeza uratibu na ushirikiano ndani ya mifumo ya pande nyingi ili kufanya kazi ya kuleta utulivu katika dunia yenye misukosuko," Xi amesema, akiongeza kuwa China inapenda kushirikiana na Belarus katika kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja na kutekeleza mapendekezo manne makubwa ya dunia yaliyotolewa na China.
Lukashenko akipongeza ushirikiano wa kivitendo wa pande zote na wa kina kati ya Belarus na China, ambao hutoa uungaji mkono muhimu kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya Belarus, amesema upande wa Belarus unaweka umuhimu mkubwa kwenye uhusiano wake na China na unatarajia kuimarisha mawasiliano ya kimkakati, kupanua maeneo ya ushirikiano, na kuhimiza uhusiano wa pande mbili upate maendeleo makubwa zaidi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



